Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti
MWANAFUNZI darasa la saba wa Shule ya Msingi ya Olmotony, Nyangusi Maiuri (15), ameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Suma JKT wanaolinda msitu wa Meru Usa uliopo wilayani Arumeru mkoani hapa.
Nyangusi alifikwa na mauti katika Kijiji cha Lengiru majira ya saa 12 jioni wakati akitoka kunywesha mifugo ya wazazi wake maji kijijini na ndipo alipokutana na askari hao, waliokuwa wakifanya oparesheni ya kukamata mifugo katika msitu huo.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Lazaro Lomayani, askari hao walipita kijijini hapo wakitoka kwenye oparesheni ya kusaka mifugo kwenye msitu huo.
Baada ya wananchi kuwaona, walianza kupiga mayowe kwa kuhofia kuvamiwa na kuanza kukimbia hovyo, hali iliyomfanya marehemu naye kukimbia na kuacha mifugo.
Ndipo askari hao walianza kufyatua risasi hovyo na marehemu alipigwa risasi kadha eneo la kiunoni na mgongoni, hali iliyomfanya kupoteza maisha papo hapo.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti alifika eneo hilo na kupokelewa na mabango ya wananchi, waliokuwa wakiandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ili kufahamu sababu zinazosababisha wananchi kuuawa ovyo.
Baada ya kufika eneo la Redio Habari Maalum, mkuu huyo wa wilaya alikutana na kundi kubwa la wananchi hao, waliokuwa wamebeba mabango, hali iliyomlazimu kutumia busara kuwaomba ili waweze kumsikiliza.
Wananchi hao waliokuwa na hasira kali, walikubali ombi la mkuu huyo wa wilaya, ambapo Mnyeti alisema serikali haikubaliani na wala haiungi mkono mauaji ya mara kwa mara yanayofanywa na askari hao wa Suma JKT.
Januari 24, mwaka huu katika eneo la Oldonyosambu Madukani, watu wanne waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine zaidi ya nane walijeruhiwa vibaya kwa risasi na askari wa Suma JKT kwa madai kuwa waliingiza mifugo katika msitu.
Baada ya mauaji hayo, polisi mkoa wa Arusha iliwatia mbaroni askari sita wa Suma JKT kwa tuhuma za mauaji hayo ya kinyama, ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, aliahidi kuwa watuhumiwa hao ambao walikaa rumande kwa siku kadhaa wangefikishwa mahakamani, lakini hawakufikishwa na haijulikani uchunguzi umeishia wapi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa mauaji ya mwanafunzi huyo na kwamba askari kadha wanashikiliwa na polisi.