Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad.
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad amesema ukaguzi wao umebaini kuwa matumizi yasiyokuwa na manufaa yenye jumla ya Sh bilioni 1.46 kwa Serikali Kuu ambayo yangeweza kuepukika kama taasisi husika zingekuwa makini.
Kwa upande wa Serikali za Mitaa, CAG alisema halmashauri 14 zililipa jumla ya Sh milioni 564.94 kwa taasisi husika.
Mfano wa malipo hayo ni tozo mbalimbali, riba na gharama za usumbufu zinazojitokeza kutokana na kesi au kutotimiza masharti ya mikataba na malipo yanayolipwa mara mbili.

Alisema imebainika pia kuwa taasisi nne za serikali kuu zilifanya malipo ya Sh bilioni 6.57 ambazo hazikuthibitishwa kupitia ukaguzi wa CAG kwa sababu zilikosa nyaraka muhimu za malipo na hivyo kushindwa kuthibitika kama fedha zilitumika kwa malengo.
Alisema ukaguzi pia umebaini upungufu katika utunzaji wa nyaraka muhimu ikiwemo nyaraka za malipo. Alisema wakati wa ukaguzi, taasisi 29 za Serikali Kuu zilifanya malipo ya jumla ya Sh bilioni 12.5, hata hivyo malipo hayo yalikosa nyaraka zinazothibitisha uhalali wa matumizi yaliyofanywa.
Utunzaji nyaraka
Kwa upande wa Serikali za Mitaa, CAG alisema ukaguzi umebaini mapungufu katika utunzaji wa nyaraka muhimu ikiwemo nyaraka za malipo zenye jumla ya Sh bilioni 9.8 hivyo kushindwa kuthibitisha uhalali wa matumizi yake.
Kwa upande wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, Profesa Assad alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh bilioni 22,495.5 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 2,642.20 sawa na asilimia 13.13 ikilinganishwa na makisio ya Sh bilioni 19.853.30 yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Alisema mapato halisi yaliyokusanywa kutoka katika vyanzo vilivyoainishwa yalifikia Sh bilioni 21,108.86 sawa na asilimia 93.84 ya makadirio ya Sh bilioni 22,495.5 ikionesha kushindwa kufikia lengo kwa jumla ya Sh bilioni 1,386.64 sawa na asilimia 6.16 ya makisio.
Alisema kati ya Sh bilioni 21, 108.86 zilizokusanywa, Sh bilioni 20,020.75 zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengineyo, matumizi ya shughuli za maendeleo na matumizi ya Mfuko Mkuu.
Alisema matumizi ya kawaida na uendeshaji wa shughuli za serikali yalifikia jumla ya Sh bilioni 15,970.12 sawa na asilimia 79.77 wakati fedha za maendeleo zilifikia kiasi cha Sh bilioni 4,050.83 sawa na asilimia 20.23.
“Hali hii inaonesha kwamba sehemu kubwa ya matumizi ya serikali yalipelekwa kwenye matumizi ya kawaida kuliko shughuli za maendeleo,” alisema CAG.
Profesa Assad alisema makadirio ya mapato na matumizi ya fedha yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka huku kukiwa na ongezeko kidogo katika kukusanya maduhuli kuweza kugharamia bajeti.
“Serikali inapaswa kuandaa bajeti yenye uhalisia kwa maana kwamba mapato ya ndani yawe na uwezo wa kugharamia bajeti kwa sehemu kubwa na kupunguza utegemezi kwenye mikopo hasa deni.”
Usimamizi wa deni la Taifa
Alisema hadi kufikia Juni 30, 2016, deni la taifa lilikuwa Sh bilioni 41,039.39 likiwa ni ongezeko la Sh bilioni 7,499.80 sawa na asilimia 22 ikilinganishwa na deni la mwaka uliopita.
Alisema kiasi hicho cha deni kilichoripotiwa Juni 30, hakikujumuisha Sh bilioni 3,217 sawa na asilimia 8 ya deni lililoripotiwa ambayo ni madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii Sh bilioni 2,991.4 na madeni ambayo hayajalipwa na yana dhana ya serikali kiasi cha Sh bilioni 225.6.
“Hii inaashiria kuwa kiasi cha deni la Taifa lililoripotiwa Juni 30, 2016, ni kidogo kuliko deni halisi. Ukaguzi umebaini kuwa serikali imeshindwa kulijumuisha deni la mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na ucheleweshaji wa kutoa hati fungani ambazo serikali iliahidi kuzitoa.
“Aidha, ukaguzi umebaini kuwa deni la Taifa linakua kwa haraka kwa zaidi ya asilimia 20 kwa mwaka ambapo kwa kiasi kikubwa inatokana na mikopo ya biashara. “Kwa maoni yangu kama ukuaji huu ukiendelea kwa kiasi cha hivi sasa bila udhibiti madhubuti utaathiri uwezo wa serikali kwenye matumizi ya maendeleo na mengineyo kwa miaka ijayo hasa ukizingatia zaidi ya asilimia 80 ya mapato yake hutumika kulipia mishahara na deni la Taifa,” alisema.
Usimamizi wa mali na madeni ya serikali
Katika eneo hilo, CAG alisema ukaguzi umebaini ongezeko la idadi ya magari yaliyotelekezwa katika taasisi mbalimbali za serikali kuu kutoka magari 675 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 1,272 mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 88.
Alisema kwa upande wa serikali za mitaa, jumla ya magari, pikipiki na mitambo inayofikia 652 yalitelekezwa pasipo hatua zozote kuchukuliwa na menejimenti.
Kwa upande wa idara na wakala wa Serikali, jumla ya magari 92 yalitelekezwa bila menejimenti na taasisi husika kuchukua hatua yoyote na uwepo wa mali hizo kwa muda mrefu pasipo kuuzwa, unaweza kusababisha hasara itokanayo na wizi wa vifaa na uchakavu.
Ukarabati wa majengo ya ubalozi
CAG alisema serikali haijachukua hatua zozote za kufanya ukarabati wa baadhi ya nyumba katika balozi za Tanzania nje ya nchi zilizo katika hali mbaya na hazifai kwa matumizi.
Alisema kati ya balozi 34, balozi 12 zinamiliki nyumba 37 zilizo katika hali mbaya na zinahitaji marekebisho wakati huo huo serikali inamiliki viwanja 10 katika balozi mbalimbali ambavyo havijaendelezwa hivyo viko katika hatari ya kunyang’anywa.
Alisema umefanyika pia uhakiki wa matumizi ya miradi ya maendeleo iliyokamilika kwa baadhi ya halmashauri na kubainika kuwa miradi yenye thamani ya Sh bilioni 4.2 ambayo haijaanza kutumika kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Alisema pia uhakiki wa dawa zilizonunuliwa kupitia fedha za Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu uliofanyika kwenye ghala la Bohari Kuu ya Dawa (MDSD) umegundua uwepo wa dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya Sh bilioni 10.187.
Usimamizi wa Manunuzi ya Mikataba
Katika eneo hilo CAG alisema katika ukaguzi huo imebainika manunuzi yaliyofanyika bila ushindani kwa serikali kuu kugharimu Sh bilioni 24.2, huku manunuzi yaliyofanyika kwa wazabuni bila mikataba kwa serikali kuu kuwa katika taasisi 10 na kuchukua Sh bilioni 11.2 na Dola za Marekani milioni 29.6.
Alisema manunuzi yaliyofanyika bila ushindani kwa serikali za mitaa yapo katika halmashauri 28 yakigharimu Sh bilioni 1.2 na manunuzi yasiyoidhinishwa ya vifaa vya matibabu bila uthibitisho wa MSD kutokuwa na vifaa hivyo kwa serikali za mitaa yapo katika halmashauri sita na kugharimu Sh milioni 72.78.
Ukaguzi wa vyama vya siasa
CAG katika eneo hilo alisema ukaguzi wa vyama vya siasa ulibaini kukosekana kwa mchanganuo wa taarifa za fedha hivyo kuweka ugumu kujiridhisha kuhusu usahihi wa taarifa hizo.
Alisema pia imebainika kuwa vyama vinne vya siasa havikuandaa taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi na wafanyakazi wa vyama vya siasa hawakuwa na mikataba huku vyama vitatu vya siasa vikiwa havina akaunti za benki.
Vyama hivyo vitatu ni Chama cha Kijamii, Chama cha Demokrasia Makini na Chama cha NRA.