RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amekutana na mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliofika kumuaga na kuwaeleza kuwa nchi zote wanazokwenda kufanya kazi ni muhimu.
Aliwataka kutambua kuwa katika ufanyaji wao wa kazi wanapaswa kujua kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina pande mbili.

Dk Shein alieleza haja ya kuimarisha uchumi wa kidiplomasia katika uwakilishi wao kwenye nchi wanakoiwakilisha Tanzania. Pia, alisisitiza waitangaze nchi na kuvutia wawekezaji katika sekta ya viwanda, pamoja na kuutangaza utalii wa nchi.
Kadhalika, aliwataka washawishi mashirika ya ndege yafanye safari zao nchini na kutaja mifano ya mashirika yanayoweza kushawishiwa kuwa ni India, Ujerumani, Algeria na nchi nyenginezo.
Kwa mujibu wa Dk Shein, ni vyema pia wakatilia mkazo umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi wa Tanzania wanasoma katika nchi wanazoenda kufanya kazi pindi wanapokuwa na matatizo.
Kwa upande wao, mabalozi hao walimshukuru Dk Shein kwa maelekezo yake na kuahidi kuyazingatia.
Mabalozi hao ni Balozi Omar Yussuf Mzee anayekwenda nchini Algeria, Balozi Dk Abdalla Possi anayekwenda Ujerumani, Balozi Baraka Luvanda aliyepangiwa India, Balozi Sylvester Ambukile anayekwenda Afrika Kusini, Balozi Job Massima anayekwenda Israel na Balozi Sylvester Mabumba atakayekuwa Umoja wa Visiwa vya Comoro.