Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi mara baada ya Kifimbo cha Malkia kufikishwa Ikulu Dar es Salaam mwaka 2014.
MICHEZO ya 21 ya Jumuiya ya Madola itafanyika Gold Coast nchini Australia mwakani na tayari maandalizi yameanza kwa ajili ya michezo hiyo.
Michezo hiyo ndio mashindano ya pili kwa ukubwa inayoshirikisha michezo mingi baada ya ile ya Olimpiki, ambayo yote hufanyika kila baada ya miaka minne. Baadhi ya nchi tayari zilianza muda mrefu maandalizi kwa ajili ya michezo hiyo na zingine zitaanza baada ya kuzinduliwa kwa mbio za Kifimbo cha Malkia wa Uingereza.

Tayari mbio hizo za Kifimbo cha Malkia zimeanza, ambapo kifimbo hicho kinabeba ujumbe maalumu wa Malkia wa Uingereza kuhusu michezo hiyo. Kifimbo hicho kitawasili nchini leo Jumamosi Aprili 8 na kinatarajia kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Ikulu, ambako kitapokewa na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kesho.
Hii mara ya nne kwa kifimbo hicho kutua nchini, ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998, kabla ya michezo ya Kuala Lumpur, Malaysia, 2002 kabla ya michezo ya Manchester, Uingereza, 2006 kabla ya michezo ya Melbourne Australia na 2014 kabla ya Michezo ya Glasgow, Scotland.
Kukimbizwa kwa kifimbo hicho ni ishara ya michezo inayofuata ya Jumuiya ya Madola, ambapo kifimbo cha mwaka huu ni ishara ya kuwepo kwa Michezo wa 21 ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia Aprili 2018. Ni utamaduni kuwa katika nchi zote kifimbo hicho kimekuwa kikipokelewa na kiongozi wa nchi husika.
Maandalizi ya Kifimbo 2017
Maandalizi ya kukipokea kifimbo hicho yalianza muda na tayari vikao vingi vimefanyika kati ya TOC, ambao ndio wenyeji wa kifimbo hicho hapa nchini pamoja na wadau wengine, zikiwemo wizara mbalimbali.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi anasema kuwa maandalizi yao yalihusisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na ile ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Bayi anasema kuwa wanahusisha wizara hizo ambazo zimetoa ushirikiano mkubwa kwa ajili ya kufanikisha mambo mbalimbali, ikiwemo usalama wakati kifimbo hicho kitakapokuwa nchini, usalama barabarani wakati kitakapokuwa kikikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Vikao hivyo vilikuwa vikiwahusisha pia wawakilishi kutoka wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambako kifimbo hicho kitatua kitakapowasili nchini leo.
Pia maandalizi ya kifimbo hicho yalihusisha Idara ya Uhamiaji, Polisi, Polisi wa Usalama Barabarani, Ubalozi wa Uingereza (kwa kuwa Kifimbo ni cha Malkia wao), Ubalozi wa Australia (licha ya kutokuwepo hapa nchini), kwa sababu wao ndio wenyeji wa michezo hiyo ya mwakani.
Bayi anasema ili kufanikisha ujio wa kifimbo hicho iliundwa Kamati ya Kikosi Kazi kwa ajili ya kufanikisha ujio wa kifimbo hicho maalumu kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Kuundwa kwa kamati
Kamati mbalimbali ziliundwa ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na kufanikisha ujio huo wa Kifimbo cha Malkia. Baadhi ya kamati zilizoundwa ni pamoja na ile ya usafiri, itifaki, kamati ya masoko, kamati ya sherehe, burudani na mapambo, kamati ya ulinzi na usalama, kamati ya habari na utangazaji na zingine.
Kwa mujibu wa Bayi, kamati hizo zimekuwa zikikutana mara kwa mara na kupitia majukumu yao ili kuhakikisha hafla ya kifimbo inakwenda vizuri kuanzia kinapowasili leo Jumamosi, kinapokimbizwa maeneo mbalimbali hadi kinapoenda Ikulu ambako kitapokewa na Rais Dk Magufuli.
Kazi kubwa ya kikosi kazi ilikuwa pamoja na mambo mengine ni kusaka fedha kwa ajili ya kufanikisha ziara hiyo ya Kifimbo cha Malkia.
Ratiba kamili ya kifimbo
Kifimbo kitawasili leo kuanzia saa 10:50 jioni kwa ndege ya Kenya Airways na kulakiwa na watu mbalimbali huku uwanjani hapo kukiwa na burudani za vikundi tofauti tofauti kabla ya kupelekwa katika Hoteli ya Southern Sun (zamani Holiday Inn), ambako kitalala.
Kesho Jumapili ndio kutakuwa na pilika pilika nyingi za Kifimbo kikianzia kutembelea studio za Azam na maeneo mengine kabla ya kwenda katika daraja kubwa na la kisasa la Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakati kifimbo hicho kikienda daraja la Nyerere, shughuli mbalimbali za burudani zitakuwa zikiendelea Uwanja wa Taifa, ambako ndiko mbio rasmi za kukipeleka kifimbo Ikulu zitakapoanzia.
Mbio za Kifimbo hicho kwenda Ikulu zitaanza Uwanja wa Taifa saa 7:00 mchana na kukimbizwa kwa saa kadhaa na kutarajia kutua Ikulu saa 10:00 jioni, ambako Rais Magufuli atakipokea kutoka kwa bingwa wa medali ya fedha wa ndondi za ridhaa wa Michezo ya Jumuiya ya Madola 1990 Auckland, New Zealand, Haji Ally Matumla.
Wenye medali wapewa nafasi Wachezaji wa Tanzania waliowahi kutwaa medali mbalimbali za Michezo ya Jumuiya ya Madola katika miaka tofauti, watapata nafasi ya kukimbiza kifimbo hicho.
Baadhi ya wachezaji hao ni pamoja na Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa, Zakayo Malekwa, Zakarie Barie, Simon Mrashani, Fabian Joseph, John Yuda, Francis Naali, Samson Ramadhani, Geway Suja na Willy Isangura. Wachezaji hao wanaifanya Tanzania kupata jumla ya medali 21 katika kipindi cha miaka 47, ambapo michezo iliyoleta medali ni ile ya riadha na ngumi za ridhaa tu.
Tanzania ina historia kubwa katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola, kwani ni michezo pekee mikubwa, ambayo imewahi kutwaa medali nyingi ukilinganisha na Olimpiki na hata ile ya Mataifa ya Afrika.
Katika mchezo ya Olimpiki, Tanzania imewahi kutwaa medali mbili tu za fedha katika mbio za meta 3,000 kuruka viunzi na maji pamoja na ile ya meta 5,000 kutoka kwa Bayi na Suleiman Nyambui mwaka 1980 mjini Moscow, Urusi. Kutokana na rekodi hizo ndio maana Tanzania ina historia ya pekee katika michezo hiyo ya Mdola kutokana na mafanikio makubwa iliyopata katika michezo.
Rekodi ya Bayi haijavunjwa Historia nyingine ya pekee kwa Tanzania katika michezo hiyo ni ile ya rekodi ya Filbert Bayi, ambapo hadi mwakani rekodi ya meta 1,500 itakuwa imefikisha miaka 44 bila kuvunjwa. Bayi aliweka historia ya aina yake duniani mwaka 1974 pale alipovunja rekodi ya dunia ya mbio za meta 1,500 kwa kutumia dakika 3:32.2.
Tanzania ina historia kubwa katika ushiriki wake wa Michezo ya Jumuiya ya Madola, ambapo ilijipatia Medali ya Fedha mwaka 1970 ikiwa ni ya kwanza, wakati wa Michezo ya Edinburg, Scotland.
Katika Historia ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, wanamichezo wa Tanzania wameweza kushinda Medali 21 (Dhahabu 6, Fedha 6 na Shaba 9) Historia ya Madola Michezo ya Jumuiya ya Madola ilianza mwaka 1930 mjini Hamilton, Canada. Kifimbo cha Malkia hukimbizwa kabla ya michezo ya Jumuiya ya Madola kuashiria kufanyika kwa michezo hiyo.
Kifimbo cha Malkia hubeba ujumbe wa Malkia ambaye ni Mkuu wa nchi za Jumuiya ya Madola kwa sasa Malkia Elizabeth wa II. Mbio kwa utamaduni huanza Buckingham, Uingereza ambapo ndipo makazi ya Malkia.
Kifimbo hicho kinakabidhiwa kwa mkimbiaji wa kwanza na kupokea kutoka mkimbiaji wa mwisho wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Jumuiya ya Madola na kusoma ujumbe uliobebwa na Kifimbo hicho cha kufungua michezo hiyo.
Michezo ya Jumuiya ya Madola ilianza kwa mara ya kwanza mwaka 1930 mjini Hamilton, Canada, lakini kwa mara ya kwanza Kifimbo cha Malkia kilianza kukimbizwa 1958, kabla ya michezo ya Jumuiya ya Madola ya mjini Cardiff, Wales.
Tangu mbio za Kifimbo cha Malkia zilipoanza hadi 1994 Kifimbo kilikimbizwa tu katika miji ya Uingereza na mwenyeji wa mashindano ya Jumuiya ya Madola tu.
Kifimbo cha Malkia kilianza kukimbizwa katika miji mbalimbali ya nchi zilizotawaliwa na Mwingereza mwaka 1998 kabla ya michezo ya Jumuiya ya Madola ya Kuala Lumpur, Malaysia, hali kadhalika mbio za mwaka 2002 kabla ya michezo ya Manchester ilikimbizwa kwa zaidi ya kilomita 100,000 kupitia miji ya nchi za Jumuiya ya Madola 23.
Kabla ya michezo ya Jumuiya ya Madola (2005) iliyofanyika Melbourne, Australia mwaka 2006 mbio za Kifimbo cha Malkia wa Uingereza zilikimbizwa kwa zaidi ya kilometa 180,000 kupitia miji yote ya nchi 71 wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Kifimbo cha Malkia huwa tofauti kila mara kinapotengenezwa, Kifimbo cha Michezo ya Gold Coast 2017 kitakuwa na GPS kufahamu Kifimbo kilipo popote duniani, Mambo mapya kabisa Mwaka huu tofauti kabisa na miaka ya nyuma, ambapo kifimbo hicho kilikuwa kikishikwa na mtu yeyote wakati wa kukimbiza, sasa kitakimbizwa na mtu mmoja kutoka katika kila kundi.
Mfano kundi la wanafunzi wa shule ya Filbert Bayi, lenyewe litakuwa na mtu mmoja atakayekikimbiza, huku wenzake wakimfuata nyuma na wakimaliza sehemu yao watakikabidhi kwa mkimbizaji wa kundi jingine huku kundi lililomaliza kukimbiza likiruhusiwa kuendelea kukimbia hadi Ikulu.
Ili kuwatofautisha, wale watakaokikimbiza kifimbo hicho wenyewe wameandaliwa fulana maalum zilizotengenezwa na waandaaji wa michezo ijayo ya Madola, Gold Coast. Wale watakaomsindikiza mkimbizaji nao watakuwa na fulana, lakini tofauti na zile za wakimbiza kifimbo, kwani zenyewe zimetengenezwa hapa hapa nchini na wadhamini wa kifimbo hapa nchini.
Njia ya Kifimbo
Mbio za Kifimbo hicho zitaanzia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kupitia Serengeti Breweries kitapita hadi Kwa Sokota, Tazara/Barabara ya Nyerere, kitapita Superdoll, Unilever, Kamata hadi katika makutano ya barabara ya Msimbazi na Uhuru.
Baada ya hapo kitapita Mnazi Mmoja, Mnara wa Saa, barabara za Samora na Morogoro, British Council, Makumbusho ya Taifa hadi Ikulu kitakapomalizia mbio zake.