Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally
WATANZANIA wamekumbushwa kuwa makini wanapokuwa wakijadili masuala mazito yenye kutoa mustakabali wa maendeleo ya nchi badala ya kufanya mzaha.
Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema hayo wakati akizungumza katika halfa yakuzindua ripoti ya utafiti wa Shirika la Hakielimu, iliyohusu utekelezwaji wa sera ya elimu bure nchini.

Alisema baadhi ya watanzania wamepoteza kiwango chao cha kufikiri ili kutoa suluhu katika masuala mazito yanayoikumba nchi, na badala yake wamebakia kujadili kwa uwepesi katika mitandao mbalimbali yakijamii, jambo ambalo haliwezi kusaidia kukuza maendeleo.
“Athari katika masuala mbalimbali hayawezi kuonekana kwa uhalisia wake, Watanzania wanapenda sana “kula ubuyu” yaani wanapenda zaidi kujadili na kusikiliza masuala ya kawaida na hata yale ambayo ni mazito huyajadiliwi kwa kina bali kwa uwepesi bila kufikia suluhu iliyo chanya,” alisema Bashiru.
Alitoa mfano kuwa suala la elimu bure nchini lingetakiwa kuzungumzwa katika kila sekta hasa ikizingatia kuwa, sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuelekea katika Tanzania ya Viwanda.
“Ilitakiwa katika utekelezwaji wa sera ya Tanzania ya viwanda, kuanza kupima ni kwa namna gani uwekezaji katika viwanda unaweza kuimarisha uchumi nchini kwa kupitia katika elimu lakini pia kuona ni kwa jinsi gani Tanzania ya viwanda inaweza kuleta mapinduzi ya elimu,” alisema Bashiru.
Alisema katika muktadha wa Tanzania ya viwanda, ni vyema ingejadiliwa kuwa ni kwa namna gani naweza kuhusiana na mabadiliko ama maboresho katika elimu, lakini pia sio kwa wawekezaji peke yake ila hata kwa sekta ya kilimo ingeweza kuahinisha uhusiano wa mapinduzi ya kilimo na uboreshwaji wa elimu nchini.