MWENYEKITI wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na mbunge wa Kawe Halima Mdee, jana wamehojiwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, inayoongozwa na Mbunge wa Newala Vijijini, George Mkuchika (CCM).
Mbowe ambaye pia ni wmenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Kawe, Mdee walitakiwa kufika mbele ya Kamati hiyo kutokana na maagizo ya Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyotoa bungeni Jumatano, Aprili 5, mwaka huu, akiwataka waripoti kwenye kamati hiyo siku iliyofuata.

Mbowe ambaye alikuwapo bungeni siku hiyo na Mdee ambaye hakuwapo, wote wawili wametii wito wa Spika, Ndugai wa kusimama mbele ya Mwenyekiti Mkuchika kuhojiwa kama ilivyokuwa imeagizwa na Spika wa Bunge wakitakiwakujibu tuhuma zinazowakabili. Mbowe inadaiwa alitoa lugha za matusi mtandaoni na Mdee anadaiwa kutoa lugha za matusi kwa Spika bungeni.
Mwenyekiti wa Chadema alifikishwa mbele ya Kamati hiyo akituhumiwa kufanya kosa la kulitukana Bunge mtandaoni baada ya wabunge wawili wa chama hicho kushindwa uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Baada ya Ezekiel Wenje na Lawrance Macha waliokuwa wakiwania nafsi za ubunge wa EALA kupitia chama hicho kupata kura nyingi za hapana, Mbowe inadaiwa alianza kutukana bunge mitandaoni.
Habari za Mbowe kwamba alitukana mitandaoni ziliibuliwa na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola (CCM) ambaye aliomba mwongozo wa Spika kuhusu kiongozi huyo kutoa lugha za matusi mitandaoni akilitukana bunge sababu ya wabunge wake kukosa kura za kutosha kuchaguliwa kuingia EALA.
Spika Ndugai wakati akitoa mwongozo kuhusu jambo hilo, alimtaka Mwenyekiti Mbowe afike kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma hizo mara moja.
Mbunge wa Kawe, Mdee, alitakiwa kujitokeza mbele ya Kamati ya Maadili kujibu tuhuma za kutoa lugha za matusi akimtukana Spika bungeni. Katika taarifa yake, Spika Ndugai alisema Mbunge Mdee, siku ya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Aprili 5, mwaka huu, alimtukana na akaamua kumnyamazia siku hiyo.
“Mdee alisikika akinitukana siku hiyo ya uchaguzi wa wabunge EALA, nikajitahidi kudhibiti hasira yangu, nikashusha hasira, nikaamua kunyamaza,” alisema na kuongeza kuwa jambo hilo liliwasikitisha wengi, wengine walimtumia ujumbe na yeye kama Spika aliamua kulipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Maadili.
Ndugai alisema huo ni mwendelezo wa kuweka na kudhibiti nidhamu ndani na nje ya Bunge hilo la Bajeti ambalo wabunge watakuwapo bungeni kwa takribani miezi mitatu.
Alisema tofauti na wakati mwingine, wakati huu mbunge mmoja mmoja atafuatiliwa na kushughulikiwa, huku akitoa tahadhari kwa wabunge wenye tabia ya kutumia lugha zisizo za staha kuziacha.
“Naanza na Halima Mdee, ambaye yeye alimtukana Spika juzi, Watanzania wengi wamesikitishwa na jambo hili, wameniandikia na kunipigia simu…hii si mara ya kwanza kwa Halima, hata juzi nilivumilia sana, nilimuomba Mungu anisaidie nikanyamaza kimya, kwa hiyo suala lake nalipeleka mara moja kwenye kamati ya maadili,” alisema.
Aliongeza kuwa, “ haiwezekani Bunge hili liwaite watu walioko nje kwa utovu wa nidhamu halafu liwafumbie macho wabunge walioko humu ndani, ambao ni watovu wa nidhamu.”
Ndugai pia alisisitiza kuwa kama Halima asiporipoti kesho yake ambayo ni Aprili 7, basi polisi imsake na kumpeleka akiwa amefungwa pingu. “Halima Mdee popote pale alipo najua hayupo Dodoma kesho muda huu awe ameripoti kwenye Kamati, kama asiporipoti akamatwe na polisi popote alipo na aletwe na pingu hapa, tumekuja mmoja mmoja na tutashughulikiana mmoja mmoja,” alisema Ndugai.
Spika wa Bunge alimuita Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti ambaye bunge hilo katika mkutano wake wa sita liliazimia aitwe kwenye kamati hiyo kwa tuhuma za kuingilia madaraka ya Bunge, aliitikia na kuhojiwa.
Maazimio yatakayofikiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, yatafikishwa kwenye ofisi ya Spika naye atatolea uamuzi au ufafanuzi mbele ya wabunge wote bungeni siku atakayoona inafaa.