Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani
SACP Onesmo Lyanga

JESHI la polisi mkoani Pwani, linamshikilia Amiri Alalae (26) mkazi wa Toptop, wilaya ya Bagamoyo kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu 30 raia wa nchini Ethiopia. 

Kamanda wa polisi mkoani humo, Onesmo Lyanga, alisema tukio hilo limetokea april 13 majira ya saa kumi usiku huko maeneo ya Kilomo kata ya Kilomo tarafa ya Yombo. 



Alieleza kuwa askari wa jeshi la polisi waliokuwa kwenye doria maeneo mbalimbali ya wilaya ya Bagamoyo walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu hao wakiwa wameingia nchini bila kibali. 

"Wakiwa wamepakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T. 824 DFG  aina ya Town hiace pickup lililokuwa likiendeshwa na Amiri Alalae "alisema kamanda Lyanga. 
Kamanda Lyanga alisema, wahamiaji waliingia nchini kwa njia ya majini wakitumia majahazi na kushukia maeneo ya bandari bubu ya Jitu Kuu kutoka nchi jirani ya Kenya. 

Alisema watawakabidhi kwa idara ya uhamiaji ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Kamanda huyo alitoa rai kwa wananchi hasa madereva kuacha tabia ya kusafirisha wahamiaji haramu kwa lengo la kujiongezea kipato. 

Alisema kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kamwe hawatakuwa na muhali na wale wote wanaofanya biashara hiyo ndani ya mkoa wa Pwani.