WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema hakuvamia mkutano wa msanii Ibrahim Mussa `Roma Mkatoliki’ na waandishi, bali ni majukumu yake kama mlezi na alikuwa ofisini kwake.

Alitoa kauli hiyo wakati akifafanua hoja mbalimbali zilizoelekezwa katika wizara yake wakati wabunge wakichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa wiki iliyopita.
Alisema alimshangaa Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliyehoji bungeni kwamba waziri huyo alikuwa anafanya nini kwenye ukumbi pembeni ya Roma Mkatoliki wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema ofisi ya wizara imehamia Dodoma katika jengo la LAPF, lakini anapokuwa Dar es Salaam ofisi za Idara ya Habari (MAELEZO) ndizo anazotumia kama ofisi yake.
Dk Mwakyembe alisema lakini pia kuna tatizo gani kuwa karibu na Roma Mkatoliki kwa sababu yeye ni waziri mwenye dhamana ya habari, utamaduni, sanaa na michezo na hivyo ni mlezi wa wasanii nchini.