MAKAMU wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya tano sasa ipo tayari kuleta nafuu baada ya hekaheka ya mwaka mzima kutafuta fedha za kuchochea uchumi.
Katika hekaheka hizo serikali ilikuwa na kazi kubwa ya kukabiliana na maadili katika ofisi zake na za umma,kukabili rushwa na ukwepaji wa kodi. Akizungumza katika hafla ya Tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora kwa mwaka 2016, Makamu wa Rais alisema kwamba serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kwamba mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa mengi yametafutiwa ufumbuzi.

Alisema mwaka wa kwanza wa serikali ulikuwa ni wa kazi nyingi na hivyo serikali ilikuwa ikitafuta fedha katika vyanzo mbalimbali vya ndani na kwamba sasa wametulia na wataleta nafuu kwa mujibu wa sheria na matakwa ya sasa ya kukuza uchumi.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais nafuu hiyo pia inatokana na ukweli kuwa serikali ipo tayari kufanyakazi na wenye viwanda kwa sababu inaamini mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuondoa umaskini, kukuza ajira na kuimarisha mwelekeo kwenda katika uchumi wa kati.
Makamu wa rais ambaye pia katika hotuba yake alikuwa anazungumzia changamoto zinazokumba sekta binafsi katika kutekeleza wajibu wake, alisema kwamba serikali ya awamu ya tano inatambua changamoto hizo na imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba zinamalizwa.
Hatua hizo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kama bandari na reli na pia kuwapo kwa kamati inayoangalia kero zinazosugua sekta ili serikali ifanye maamuzi na kutoa maelekezo.
Alisema baadhi ya kero kwenye sekta nyingine kama ya kilimo zimefanyiwa kazi. Kero hizo ni panmoja na kuondoa tozo kadha kwenye zao la chai, pamba na kahawa. Aidha alisema kwa sasa kuna kamati inayoangalia namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara inayofanyakazi chini ya Wizara ya Viwanda, biashara na uwekezaji na kuitaka imalize kazi yake mapema na kuikabidhi serikali kwa hatua zaidi.
Akimkaribisha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili amkaribishe Makamu wa Rais kuzungumza na washiriki katika hafla hiyo,Makamu wa pili wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Shabbir Zavery alitaja changamoto tisa zinazotia msukosuko ukuaji wa viwanda nchini.
Moja ya changamoto hizo ni mabadiliko ya mara kwa mara na ya ghafla ya sera au sheria za kibiashara ambayo huondoa utulivu kwa wazalishaji.
Zavery alisema kwamba ufanisi na utuilivu wa kufanya biashara unategemea sana kutobadilika kwa mara kwa mara kwa sheria na sera za biashara na mwaka uliopita serikali ilichukua maamuzi kadhaa bila kuhusisha sekta binafsi na hivyo kudhoofisha ushirikiano baina ya serikali na wafanyabiashara.
Alisema pia kuwapo kwa utitiri wa mamlaka za udhibiti na tozo zao mbalimbali ambazo pia zinafanyakazi zinazofanana na kutembelea viwanda kwa kila mamlaka kwa wakati wake, kunachangia gharama za kufanyabiashara.
Akizungumzia tatizo sugu la wenye viwanda na wafanyabiashara kutorejeshewa malipo stahiki (Vat na nyinginezo) wanazodai kutoka Mamlaka ya Kodi, na kodi zinazoua ushindani,Makamu wa Rais Samia amesema kwamba serikali kwa sasa imeshatulia na kwamba itaendelea kufanya marejesho kwa mujibu wa sheria na suala la kodi zenye kero limeshafanyiwa maelekezo na kwamba wahusika wanatakiwa kukutana kushughulikia tatizo hilo.
Aidha ameiagiza Wizara ya viwanda , biashara na uwekezaji kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mikakati ya kupunguza kero kwa wawekezaji na wafanyabiashara inatekelezwa kwa vitendo.
“Nafahamu kuwa sekta ya viwanda imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali. Serikali tunaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha viwanda vyetu vinakuwa katika mazingira rafiki na wezeshi ili kuwaongezea ufanisi na ushindani katyika masoko ya kimataifa,” alifafanua makamu wa Rais.
Makamu wa Rais pia alikumbushia maneno aliyotoa katika ziara zake mikoani hivi karibuni kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kukaa, kujadili na kuona namna ya kuondoa adha katika uwekezaji na ufanyaji biashara bila kuipotezea mapato serikali.
Aidha alisema kwamba wakati serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zinazoathiri ukuaji wa sekta ya viwanda, ni muhimu pia kwa wawekezaji na wazalishaji kutambua majukumu yao katika kuchangia juhudi hizo.Alisema majukumu hayo ni pamoja na kuzalisha bidhaa nyingi , zenye ubora na zenye bei rafiki kwa mlaji.
“Tusisahau kuwa sekta ya viwanda ina jukumu kubwa sio tu la kuipatia serikali mapato; bali pia kutoa ajira kupunguza umaskini pamoja na kuijengea nchi heshima kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na ushindani wa kimataifa” alisema Makamu wa Rais.
Aliiagiza wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji kuratibu na kukutana na wizara au taasisi za serikali na za umma nchini ili kuwahamaisha kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kama ilivyoanza kwa vikosi vya usalama ambapo wanatakiwa kununua bidhaa zao hapa nchini.
Aliwatakaa pia wafanyabiashara kuingia ubia na mifuko ya jamii ili kuwa na mitaji itakayowezesha kuanzisha viwanda kwa pamoja. Katika tuzo hizo mshindi wa kwanza wa jumla alikuwa ni Tanzania Breweries Limited, akifuatiwa na Mufindi paper Mills Company limited na mshindi watatu alikuwa Kioo Limited.
Aidha kulikuwa na washindi katika viwanda vidogo vya kati na vikubwa. Mshindi katika safu ya viwanda vidogo wa kwanza alikuwa Alliance Life Assurance Limited kwenye masuala ya fedha na bima na mshin di mwingine alikuwa ni Prisons Corporation Sole katika bidhaa za ngozi na viatu.
Kwa viwanda vya kati katika hafla hiyo ambayo mdhamini wake mkuu ni Bank M, mshindi katika ujenzi alikuwa Dharam Singh Hanspaul and Sons Limited; safu ya kemikali mshindi alikuwa Royal Soap and detergent Industries Limited; katika nishati ,umeme na elektroniki mshindi alikuwa Tanalec Limited na katika usindikaji wa chakula mshindi alikuwa Chemi Cotex industries limited.
Washindi wengine viwanda vya kati walikuwa Ital Shoe Limited katika bidhaa za ngozi na viatu; Chemi Cotex Industries limited katika bidhaa za metali ;Nyanza Mines (T) Limited katika bidhaa za madini; Hanspaul Automechs Limited safu ya magari na vifaa vyake; Tanpack Tissues limited bidhaa za karatasi na makasha na DPI Simba Limited katika safu ya bidhaa za plastiki.
Kwa viwanda vikubwa washindi katika nafasi mbalimbali ni Tanzania Breweries limited, Petrolube (T) Limited, Petrofuel (T) Limited, Alliance Insurance Corporation Limited, Said Salim Bakhressa, Alaf Limited, Kioo Limited, Mufindi paper Mills Company Limited, Jambo Plastics na Nida Terxtile Mills (T) Limited.
Washindi wa tuzo hizo walipatikana kwa kuzingatia ufanisi katika uzalishaji, mauzo ya nje, uwekezaji katika teknolojia ya kisasa,matumizi bora ya nishati, utunzaji wa mazingira, afya na usalama wa wafanyakazi, uwiano wa kijinsia katika uongozi, pamoja na mchango katika jamii.