WATU wanne wanaosadikiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi wanane na uporaji wa silaha katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani wameuawa na polisi wakati wa operesheni iliyofanywa baada ya tukio hilo.
Aidha, Jeshi la Polisi limetaja chanzo cha mauaji ya askari polisi kujirudia mara kwa mara katika maeneo hayo ya kuanzia Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti ni eneo ambalo lina watu wachache, lakini kuna mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye nia mbaya kujificha.

Akizungumza kuhusu tukio hilo katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema baada ya majambazi hao kuwaua askari hao walipora bunduki saba na kutokomea kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo polisi walifanya operesheni na kufanikiwa kutambua maficho ya muda ambapo katika majibizano ya risasi walifanikiwa kuwaua watu hao wanne pamoja na kupata silaha nne mbili zikiwa ni za askari waliouawa na mbili za majambazi hao.
“Mpaka sasa nimeshapoteza askari zaidi ya 10 ninaamini wanatosha, kuanzia sasa jeshi linakwenda kwenye operesheni maalumu, hatutokuwa na mzaha, hatutokuwa na msamaha, tutakwenda kufanya kile ambacho jeshi linapaswa kufanya, tutawapata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu na hakuna atakayebaki,” alisema Mssanzya.
Alisema mapambano hayo hayana mwisho kwa kuwa askari 10 ni wengi na kuwataka wananchi kuwawia radhi na kuwaunga mkono, kwani katika hilo wataona sura halisi ya jeshi hilo.
Mssanzya pia alitoa onyo kwa watu wengine waliokuwa wakifikiria kufanya ujambazi wa kutumia silaha kuwa wajue kuwa dawa ya moto ni moto, hawatamvumilia mtu yeyote.
Akijibu swali kama tukio hilo lina viashiria vya ugaidi, Mssanzya alisema, tukio hilo haliwezi kuwa la kigaidi, bali ni uhalifu wa kawaida, akisema nchi hii haina ugaidi kwani nchi yenye ugaidi haiwezi kuwa na amani.
“Watapatikana hivi karibuni na watajua tofauti ya moto na maji… tumefuatilia jana (juzi) na imekuwa nane kwa nne muda si mrefu hesabu yetu itakuwa kubwa kuliko ya kwao, wiki hii ikipita magoli yetu yatakuwa mengi kuliko ya kwao na tutaendelea hivyo hivyo,” alisema.
Aidha, alipiga marufuku pikipiki kutembea zaidi ya saa 11 jioni katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji wakati operesheni hiyo ikiendelea.
Kauli za Waziri Mwigulu
Akizungumza jana na gazeti hili kufuatia vyombo vya kigeni kusema askari polisi kushambuliwa na kuporwa silaha ni kawaida nchini, Waziri wa mambo ya Ndani,Mwigulu Nchemba alisema matukio ya kihalifu ya aina hii hayajazoeleka na wala si ya kawaida.
Aidha, alisema shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kutokana na kazi nzuri inayofanywa na askari Polisi katika kukabiliana na makundi ya kihalifu ambayo yanajificha ndani ya misitu katika maeneo ya Kibiti.
Amesema kutokana na matukio kadha katika maeneo hayo ya Kibiti, Polisi walianza kazi nzito ya kukabiliana nao na hivyo kitendo walichofanya usiku wa kuamkia jana ilikuwa ni kulipiza kisasi baada ya kusukumwa kutoka katika maeneo waliyozoea kukaa na kufanya shughuli zao za kihalifu.
Akiwa katika eneo la tukio, waziri Mwigulu alisema alisema tukio lililotokea sio taarifa njema na ni jambo baya kwa Tanzania na Ukanda huo ambao umekuwa na matukio mengi ya mauaji.
Aliongeza kuwa tukio hilo limeifanya serikali kuangalia namna mpya ya kujipanga kukabiliana na matukio hayo ambayo yameendelea kugharimu maisha ya askari.
“Tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha uhalifu wa aina hii haupati nafasi katika ukanda huu na kanda nyingine na niseme tu wale wote waliohusika kufanya vitendo hivi hawatavumiliwa na tutahakikisha wanalipa, hatuwezi kukubaliana na tutahakikisha tunapambana kurudisha silaha zetu na kuwakamata wote waliohusika,”alisema Mwigulu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema tukio hilo ni la kusikitisha na sio la kufumbiwa macho.
Alisema katika kuhakikisha wanakabiliana na matukio hayo ofisi yake pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani watasajili upya wananchi wanaojishughulisha na uchomaji mkaa kwa kuwa matukio mengi yanayofanyika wahusika wanakimbilia katika maeneo ya wachoma mkaa.
“Tumeongea hapa na Waziri ili tuwasajili upya watu hawa wanaochoma mkaa kwakuwa wakiwa na leseni tutaweza kuwatambua na wale wataokimbia katika maeneo hayo baada ya kufanya matukio iwe rahisi kuwapata kwa kuwa baada ya tukio wamekuwa wakikimbilia katika maeneo hayo,”alisema.
Ndikilo pia amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa na tabia ya kushirikiana na jeshi la polisi ili kuhakikisha wanadhibiti uhalifu huo, kwani wananchi wengi wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.
Alisema baada ya kutembelea eneo la tukio wamebaini wahusika walikaa katika eneo hilo zaidi ya siku tano kwa kuwa walikata baadhi ya miti ambayo tayari imekauka, hivyo kungekuwepo na ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo wangeweza kupata taarifa mapema na kudhibiti tukio hilo.
“Bado tunajiuliza hatujui hawa wananchi wana hasira gani na jeshi la polisi wamekuwa hawatoi ushirikiano hata kama mhusika yupo katika eneo lake hatuelewi ni sababu za kisiasa au kiuchumi hatujui,” aliongeza Ndikilo.
Aidha Ndikilo ameliomba jeshi hilo kuongeza askari katika eneo hilo ambalo lina mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye nia mbaya kufanya matukio na kujificha.
Hali ilivyo katika eneo hilo Katika eneo hilo wananchi walionekana kujawa na hofu kubwa huku wengi wakihofia usalama wao.
Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake mkazi wa eneo hilo alisema matukio hayo yamekuwa ni ya kujirudia, hivyo wameiomba serikali kuongeza nguvu katika eneo hilo.
“Naogopa hata kuzungumza na wewe nisije nikaonekana sababu hapa ukizungumza na waandishi wa habari wakikugundua wanakutolea vitisho na wengine hadi wanauawa tunaomba sana jeshi la polisi kuhakikisha wanaongeza nguvu katika eneo hili kwa kuwa sasa tunaogopa sijui kama wakimaliza kwa askari watakuja kwetu,”alisema Mwananchi huyo.
Chanzo cha matukio
Akizungumzia chanzo cha matukio ya mara kwa mara ya mauaji ya askari alisema, maeneo hayo bado yana watu wachache lakini kuna mapori makubwa ambayo yanatoa nafasi kwa watu wenye nia mbaya kujificha na ndio sababu hupatikana maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mssanzya, majambazi hao waliweka mtego na kulishambulia gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba PT 3713 lililokuwa limewabeba askari tisa waliokuwa wakitoka kazini eneo la Jaribu Mpakani kurejea kambini na kuwaua askari nane na kumjeruhi mmoja kisha kupora bunduki.
Alisema askari hao walikuwa wanatoka kubadilishana lindo ndipo waliposhambuliwa kwa kupigwa risasi katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi na kisha majambazi hao kupora bunduki saba zikiwemo SMG nne na Long Range tatu.
Aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, F 3451 koplo Francis, F 6990 PC Haruna, G 3247 PC Jackson, H 1872 PC Zacharia, H 5503 PC Siwale, H 7629 PC Maswi na H 7680 PC Ayoub.
Matukio ya kuuawa kwa askari polisi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ambapo katika miaka ya hivi karibuni kumetokea mauaji ya polisi katika maeneo ya Mkuranga, Ikwiriri, Mbande na Kibiti ambapo zaidi ya askari 10 wameuawa katika matukio hayo.
Rais Magufuli anena RAIS John Magufuli amelaani tukio la kushambuliwa na kuuawa askari polisi wanane na watu wenye silaha juzi jioni katika eneo la Jaribu Mpakani, wilayani Kibiti, Mkoani Pwani.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Mgiswa jijini Dar es Salaam ilisema Rais amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari hao na kulaani matukio ya kushambulia polisi wanaofanya kazi kubwa ya kulinda raia na mali zao.
Kufuatia vifo hivyo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, askari polisi wote na watanzania wote walioguswa na vifo vya polisi hao waliokuwa wakitoka kubadilishana doria na kushambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.
“Nimeshitushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu nane ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia taifa, naungana na familia za marehemu wote, jeshi la polisi na watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu… namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alilaani matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na kuwataka Watanzania wote watoe ushirikiano ili kukomesha vitendo hivyo na kuwaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi.
Chama cha ACT
CHAMA cha ACT Wazalendo kimetuma salamu za pole kwa familia, jeshi la polisi na Mkuu wa Jeshi hilo Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu kufuatia vifo vya askari wanane waliouawa juzi huko Jaribu Mpakani,wilayani Kibiti.
Katibu, Kamati ya Amani na Usalama - ACT Wazalendo, Mohammed Babu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana alisema chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kushambuliwa na kuua askari hao na kuwataka Watanzania kushikamana wakati huu wa majonzi ya kupoteza askari hao.
“ACT Wazalendo tunaungana na wito wa kuwataka watanzania kushikamana na vyombo vya ulinzi na usalama kipindi hiki cha majonzi kwa Taifa pamoja na kutoa ushirikiano kwao kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa,” alisema Babu katika sehemu ya taarifa yake.
Babu alisema kitendo hicho ni shambulio dhidi ya Jamhuri na kwamba hatua kali na madhubuti zinapaswa kuchukuliwa na kuongeza kuwa mlolongo wa matukio ya namna hiyo unaonesha nchi inapambana na kundi lisilo la kawaida na hivyo weledi wa hali ya juu unatakiwa katika kukabiliana na tishio hili dhidi ya taifa.
“Jeshi la polisi linatakiwa kufanya kazi zake kwa uangalifu mkubwa na kuepuka kabisa na kuwaingiza raia wasio na hatia kwenye mateso yeyote, kwani adui asipopatikana madhara yake ni makubwa zaidi. Matukio ya aina hii katika miezi ya hivi karibuni yawe funzo katika kukabiliana na uhalifu kama huu… tunatahadharisha kutotumia mwanya huu kuingiza wasiohusika kwani kufanya hivyo ni kuwapa ushindi wahalifu,” alisema.
Babu alisema ACT Wazalendo ina tumaini polisi itahakikisha inawasaka, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria wote waliohusika na mauaji askari hao askari wetu waliokuwa katika majukumu yao ya kikazi.
Tume ya Haki yalaani
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) nayo imesema imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuuawa kwa askari wanane wa Jeshi la Polisi, katika tukio lililotekelezwa na watu wasiofahamika jioni ya Aprili 13, 2017 katika kijiji cha Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema Tume inalaani vikali mauaji hayo ya kikatili ya askari polisi waliokuwa kazini na wasiokuwa na hatia na kwamba wanaungana na watanzania wengine kuwapa pole familia za wafiwa na Jeshi la Polisi kwa ujumla.
Alisema kumbukumbu zinaonesha kuwa matukio ya mauaji ya askari polisi na wananchi wengine maeneo tofauti mkoani Pwani tangu mwaka 2015 yamekuwa yakiongezeka na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu, hususan haki ya uhai inayolindwa na Katiba ya nchi na madhara mengine kwa familia za wahanga, kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Alisema haki ya kuishi kama zilivyo haki nyingine, inalindwa kisheria na pia inalindwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia na kuwa hakuna mtu anayepaswa kuporwa haki hii ya msingi kiholela.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 14, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Alisema ikumbukwe kuwa askari polisi wanapokuwa kazini wanatekeleza majukumu muhimu ya kulinda raia na mali zao, kwa hiyo usalama wao unategemewa na Watanzania wote na kuwa yeyote anayewaua askari polisi siyo tu anataka kuwachonganisha askari polisi na raia, bali pia anawaweka raia hao katika hofu kubwa ya usalama wao na mali zao.
Nyanduga alisema kutokana na matukio hayo tume inashauri kuhakikisha kuwa haki ya kuishi ya askari polisi na wananchi wote inalindwa, polisi na Serikali kwa ujumla wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini sababu za mauaji haya kutokea kwa kujirudia mkoani Pwani na kuhakikisha wahusika wote wanapatikana na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili sheria ichukue mkondo wake.
Imeandikwa na Katuma Masamba na Sophia Mwambe.