TANZANIA imetajwa kuwa kinara katika kudumisha uhusiano mzuri na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa. Katika kuendelea kuimarisha na kupanua uhusiano na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa, katika mwaka 2016/17, Tanzania imefungua balozi mpya sita katika nchi mbalimbali duniani.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizitaja nchi ambazo Tanzania imefungua balozi mpya kuwa ni pamoja na Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki, lakini pia mbali na kufungua balozi hizo, mabalozi wake wameteuliwa na kupangwa ili kuendeleza uhusiano wa Tanzania na nchi hizo na jirani.
Akisoma bajeti ya ofisi yake, mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu Majaliwa alisema, uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali duniani na mashirika ya nje ni moja ya misingi ya sera ya mambo ya nje ya nchi.
“Tumeendelea kuimarisha ujirani mwema baina yetu na nchi jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kutokana na kudumisha uhusiano huo, alitoa wito kwa mabalozi wa Tanzania katika balozi mbalimbali duniani, kuendelea kuitangaza nchi kama eneo mwafaka lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.
Waziri Mkuu alisema balozi hizo zina kazi kubwa ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na raslimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ukizingatia utulivu na amani iliyopo.