Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki anawataka wabunge wa chama cha ANC kutenda yatakayowafaa raia na sio kile kitakachofaidi chama, wakati wa kujadili mswada wa kutokuwa na imani na rais Jacob Zuma, wiki ijayo.

Wito wa Mbeki huenda ukawakera wanaomuunga mkono Zuma ambao wameapa kuupinga mswada huo vikali bungeni, kulingana na tovuti ya IOL.
Upinzani unadai kuwa Zuma ni mfisadi na kuwa alimfuta kazi Pravin Gordhan kama waziri wa fedha, licha ya kuwa Gordhan aliheshimika sana. Wanasema nia ya Zuma ilikuwa kuchukua usukani katika wizara ya fedha.
Zuma anakanusha madai ya ufisadi akisema kuwa yeye kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri ni kwa manufaa ya raia
Kulingana na tovuti hiyo, Mbeki alisema kuwa wabungewanafaa kuwa sauti ya wananchi na wala sio sauti ya vyama vya kisiasa. Anasema huu ni wakati wa Afrika Kusini kujua kweli uhusiano wa kikatiba kati wa wananchi na viongozi wao wa kisiasa.
Mbeki ni mwanachama wa ANC ambaye alijiuzulu kama rais baada ya kupoteza imani kwa chama hicho kinachoongozwa na Zuma, mwaka wa 2008.