ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi akizungumza na wanafunzi kutoka shule mbalimbali Jijini Tanga wakati wa uzinduzi wa Juma la Elimu wilaya ya Tanga ambapo kiwilaya lilifanyika kwenye shule ya Sekondari Tanga Don Bosco iliyopo eneo la Maweni jijini Tanga inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga.
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi wa pili kulia  akimkiliza mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo wakati alipokuwa akifafanua jambo
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi katikati akionyesha jambo na Sista ambaye anafanya kazi kwenye shule hiyo
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi amesema iwapo Serikali inataka nchi ya viwanda hawana budi kuweka msukumo mkubwa kwenye kupiga vita dawa za kulevya vitendo ambazo zimechangia kwa asilimia kuwaharibu vijana wengi hapa nchini. 

Banzi aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Juma la Elimu wilaya ya Tanga ambapo kiwilaya lilifanyika kwenye shule ya Sekondari Tanga Don Bosco iliyopo eneo la Maweni jijini Tanga inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga. 

Alisema ili kutimiza azma hiyo ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa  nchi lazima kuwepo na juhudi kubwa za kuuteketeza mtandao wa dawa za kulevya hapa nchini uliyoharibu vijana wengi ambao wangekuwa nguvu kazi  kubwa ya Taifa la kesho. 

“Kama tunataka kuifanya nchi kuwa ya viwanda maana yake kila mmoja apate elimu ya madhara ya dawa za kulevya lengo kubwa likiwa kuliondoa tatizo hilo kwa vijana ambalo limekuwa likipoteza nguvu kazi ambayo ingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali lakini pia kuwepo kwa mapambano ya kupiga vita hali hiyo “Alisema. 

“Lazima kuwepo kwa dhamira ya dhati na mipango ambayo itawezesha kuutokomeza mtandao wa dawa za kulevya unaoangamiza vijana wengi ambao wangewezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kujiingizia kipato halali na kuendesha maisha yao bila kuwa tegemezi “Alisema Askofu Banzi. 

“Vijana tuachane na matumizi ya dawa za kulevya ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha kuharibu vijana ili kuendana na sera ya maendeleo ya viwanda kwa kuyapiga vita”Alisema. 

Akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira,Askofu Banzi aliitaka
jamii kuacha kukata miti ovyo,kuchimba mahandaki ambayo kwa asilimia kubwa yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira. “Kwani suala la ukataji miti ovyo limekuwa tishio kubwa hapa nchini na kuifanya kugeuka jangwa kitendo ambacho kimeweza kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira kwa jamii hivyo lazima tuachana na jambo hilo“Alisema. 

Awali akizungumza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Don Bosco Gregory Mhuza alisema waliamua kupanda miti ili kuhakikisha wanatunza mazingira ambayo ni muhimu kwa jamii. 

“Sisi kama shule leo hii tumepanda miti lakini tutahakikisha
tunaitunza na kuilinda kwa vizazi vya sasa na vijazo ili kuiepusha
nchi yetu kukumbwa na janga “Alisema. 

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Maweni,Wales Janga alisema uzinduzi wa Juma la Elimu kwa kupanda miti katika shule hiyo ni ishara ya kuthamini uwepo wa mazingira kutokana na usemi usemao tunza mazingira yakutunze hivyo jamii haina budi kufanya hivyo ili kuendena na suala hilo.

“Pamoja na kupanda miti pia tutatembelea maabara ya ufundi kwani shule hii ni shule ya Ufundi ili tuweze kuona namna vijana wetu wanajifunza katika masomo yao ya ufundi kuelekea Tanzania ya Viwanda ya Mwaka 2025 “Alisema. 

Alisema kauli mbiu hiyo inalenga kuikumbusha jamii majukumu yake katika suala zima la elimu duni kwani baadhi yao wamelipokea suala la elimu bila malipo tofauti na kujisahau kuwa wao ni mdau namba“Alisema.


Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii Tanga Raha.