Waziri Asiye na Wizara Maalumu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ada- Tadea, Ali Juma Khatib
VIONGOZI wametakiwa kuiga mfano wa Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume katika kuwajibika kwa kuweka mbele uzalendo wa taifa na kupambana na ubinafsi ambao ni sumu ya maendeleo.

Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Karume, Kisiwandui mjini Unguja, Waziri Asiye na Wizara Maalumu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ada- Tadea, Ali Juma Khatib alisema vigezo vya uwajibikaji wa hayati Karume vinaonekana hadi leo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kisasa za maendeleo zilizojengwa Unguja na Pemba hadi vijijini.
Alisema kiongozi mzalendo ni yule anayefanya kazi kwa kuweka maslahi ya taifa mbele, mambo ambayo hayati Karume yote aliyatekeleza na kuyasimamia kikamilifu kwa nguvu zake zote.
Kwa mfano alisema mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, hayati Karume alitangaza elimu bure kwa wananchi wote wa Zanzibar Septemba 23, 1964 huku akipiga marufuku shule zilizokuwa zikitoa elimu kwa misingi ya ukabila.
Aidha alisema kubwa zaidi ni kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26 mwaka 1964 ambao ndio kielelezo kikubwa cha taifa hili kwa kutoa nafasi kubwa kwa wananchi wa pande mbili hizi kuishi bila ya ubaguzi wala bughudha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema wananchi wa Zanzibar hawatamsahau hayati Karume kwa kuwapatia eka tatu ambazo zinatumika hadi leo kwa shughuli za kilimo.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya (CCM) Zanzibar, Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu alisema Karume ataendelea kukumbukwa kwa sababu ya uwajibikaji wake na nia ya dhati ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Parmukhi Hoogan Sikh alimtaja hayati Karume kuwa kiongozi aliyeweka pembeni tofauti za dini, ukabila na kuwaunganisha wananchi kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Fatuma Said (30) ambaye alizaliwa bila ya kumfahamu hayati Karume alisema anamkumbuka kwa kuona mambo makubwa yaliyofanywa ikiwemo ujenzi wa nyumba za maendeleo zilizojengwa hadi vijijini za ghorofa.
Hayati Karume aliuawa na wapinga maendeleo tarehe 7 Aprili , mwaka 1972 wakati akiwa amepumzika na viongozi wengine wa chama cha ASP Kisiwandui mjini Unguja na ndio sehemu ulizikwa mwili wake.