Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (kulia) akiwa na kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Wambura Sabora wakati Mkurugenzi Mkuu huyo wa NBS alipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kuangalia jinsi zoezi la Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI linavyoendelea.
  Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (katikati) akiwa na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kukinga na Kuzuia Magonjwa (CDC) Dkt. Eunice Mmari (kulia) wakipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wadadisi wanaofanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Bw. Johnmark Obura wakati wa ziara iliyofanyika mkoani Kagera hivi karibuni kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
 Mdadisi Bi. Shinuna Said akichukua damu kwa mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera hivi karibuni kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI unaofanyika nchi nzima.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ICAP Tanzania Dkt. Fernando Morales (katikati) pamoja na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kukinga na Kuzuia Magonjwa Tanzania (CDC) Dkt. Eunice Mmari (kushoto) wakiangalia jinsi Mdadisi Bi. Shinuna Said (hayupo pichani) anavyochukua damu kutoka kwa mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera hivi karibuni kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI  wakati wa ziara iliyofanyika mkoani humo kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akimuhoji mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kuhusu jinsi zoezi la Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI  lilivyofanyika katika kaya yake. Mahojiano hayo yamefanyika  wakati  Mkurugenzi Mkuu huyo wa NBS alipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
Mdadisi Bw. Johnmark Obura akihojiwa na baadhi ya waandishi wa habari kuhusu jinsi zoezi la Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI linavyofanyika mkoani Kagera wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa iliyofanyika hivi karibuni kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
Na: Veronica Kazimoto
Imeelezwa kuwa asilimia 97 ya watanzania wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI katika mikoa 11 ambayo imeshafikiwa hadi sasa,  wameshiriki kikamilifu katika utafiti huo unaoendelea kufanyika nchini.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa utafiti huo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Wambura Sabora alipofanya ziara mkoani humo kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
"Ninayo furaha kukutaarifu kwamba,  mpaka sasa utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara pamoja  na visiwa vyote vya Zanzibar yaani Pemba na Unguja.  Jambo la kufurahisha zaidi ni mwitikio wa wananchi ambao ni asilimia 97 ya wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya utafiti kukubali kushiriki," amesema Dkt. Chuwa.
Mikoa ambayo imekamilisha utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI ni pamoja na Singida, Dodoma, Manyara, Iringa, Njombe na Ruvuma. Mikoa mingine ni Mbeya, Songwe, Katavi, Tabora na Kigoma.
Nae Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Wambura Sabora amemwambia Mkurugenzi Mkuu wa NBS kwamba, zoezi la utafiti huo mkoani humo linaendelea vizuri na mpaka sasa hakuna tatizo lolote  lililoripotiwa ofisisini kwake.
"Nami nichukue fursa hii kukueleza kwamba zoezi hili linaendelea vizuri hapa mkoani Kagera na mpaka sasa hakuna shida yoyote iliyojitokeza. Aidha, maeneo ya Kerwa, Missenyi na Wilaya ya Bukoba tayari yamekamilisha utafiti huu", amesema Sabora.
Kwa upande wake  mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera aliyehojiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina Chuwa kuhusu jinsi alivyoshiriki kwenye utafiti huo, alisema amefurahishwa na utafiti huo kwa kuwa amepata fursa ya kupima vipimo mbalimbali ambavyo hakutarajia kuvipata vyote kwa wakati mmoja.
"Kwakweli nimefurahishwa na utafiti huu kwakuwa sikutarajia kupima vipimo vya magonjwa ya Homa ya Ini, Kaswende pamoja na UKIMWI kwa wakati mmoja nikiwa nyumbani kwangu," ameeleza Mkazi huyo wa kijiji cha Chonyonyo.


Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC)