Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga ametaja maeneo muhimu matano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel, yatakayofanyiwa kazi baada ya ziara ya kuitembelea nchi hiyo na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu.

Maeneo yaliyobainishwa katika ushirikiano huo ni sekta za kilimo, afya, utalii, ulinzi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Balozi Mahiga aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya ziara yake aliyoifanya nchini Israel hivi karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza azma ya Taifa hilo kubwa duniani kuisaidia Tanzania bila masharti yoyote.
Alisema kwa upande wa sekta ya kilimo, wameona ni jinsi gani nchi hiyo imeweza kugeuza jangwa kuwa eneo la kilimo kwa utaalamu. Alisema mfano ni jinsi nchi hiyo ilivyobadili tabia nchi ya jangwa kuwa sehemu ya kilimo katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 80. Aliongeza kuwa nchi hiyo haina mvua na wanaweza kukaa miaka mitano bila mvua, lakini wamebuni namna ya kupata maji kwa kubadilisha maji ya chumvi ya bahari kuwa maji na kwa utaaalamu huo wanapata maji ya kutosha kuuza kwa nchi jirani.
“Ukitazama utaalamu huu na kilimo cha umwagiliaji, hicho ndicho tunachokihitaji sisi Tanzania, maeneo mengine nchini hatuna shida ya mvua lakini katikati ya nchi yetu tuna shida ya mvua isiyotosha na kutokana na mabadiliko ya tabia nchi inazidi kuwa kame, nadhani katika eneo hili suala la kilimo na maji Israel wanaweza kutusaidia sana,” alisema Mahiga.
Alisema kwa kuona umuhimu wa sekta hiyo ya kilimo, nchi hiyo ipo tayari kuchukua Watanzania 200 kwa ajili ya kupata mafunzo ya kilimo. “Netanyahu alitushangaa hapa akasema watu wanaokuja kusoma kutoka Tanzania wapo 45 tu, lakini kutoka Uganda wapo 200, Kenya 150, ninyi kwanini mpo wachache na kusema wao wapo tayari kuchukua zaidi ya watu 200 pamoja na kuleta wataalamu kuja kufundisha kilimo hapa nchini,”alisema. Akizungumzia eneo la ulinzi na usalama, Mahiga alisema Israel ipo vizuri katika jeshi lake na wana mbinu zenye manufaa hivyo wanaweza kushirikiana na Tanzania hata kwa kutoa mafunzo hasa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Pia alisema sekta nyingine ambayo wanaweza kushirikiana ni sekta ya utalii, ambapo alisema licha ya nchi hiyo kutokuwa vizuri na Tanzania kwa muda mrefu lakini watalii walikuwa wanakuja na mwaka huu watalii kutoka Israel wamefikia 50,000 na angependa kuona idadi hiyo inaongezeka ilimradi wawe na usalama pamoja na kuwepo kwa matangazo zaidi juu ya sekta hiyo. Alisema sekta nyingine ambayo wameona wanaweza kushirikiana na Tanzania ni Tehama kwa kuwa nchi hiyo ipo mbali katika sekta hiyo hasa katika utengenezaji wa vifaa na elimu ya Tehama.
“Kama mmewahi sikia ndege zisizo na rubani ni wao wametengeneza na wana utalaamu wa ulinzi dhidi ya mitandao yao, sasa niseme wamesema wapo tayari kufundisha wataalamu wa hapa nchini katika sekta hiyo,”aliongeza Mahiga. Kwa upande wa sekta ya afya, alisema wataendelea kushirikiana hasa kwa kupeleka madaktari kusoma Israel pamoja na kuleta wataalamu na kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita waliweza kusaidia wagonjwa wa moyo wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zaidi ya 24,000 na kuokoa kiasi cha Sh bilioni 70 ambazo zingetumiwa na serikali kupeleka wataalamu nje ya nchi. Alisema mbali na kutoa wataalamu, Israel wana mpango wa kuigeuza Taasisi ya JKCI kuwa bingwa katika nchi zilizopo katika Jangwa la Sahara. Akizungumzia uwekezaji ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda, alisema Waziri Mkuu huyo alisema nchi yake ipo tayari kuwekeza Tanzania na mwakani atakuja nchini, akiambatana na ujumbe wa uwekezaji katika sekta zote.