MFUMO wa kidijitali wa kufuatilia treni ya abiria na ya mizigo, uliozinduliwa na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mwishoni mwa wiki iliyopita, umeifanya mamlaka hiyo kuwa juu na inayoendeshwa kisasa zaidi katika Afrika Mashariki.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Meneja Mkuu wa Tazara Kanda ya Tanzania, Fuad Abdallah amesema wataalamu wa Tehama wamefanikiwa kutengeneza mfumo unaofuatilia mwenendo wa treni kutoka mwanzo wa safari mpaka mwisho. Alisema siyo mara ya kwanza kwa mfumo huo, kutumika hapa nchini. Alisema hapo awali ulikuwa ukitumika mfumo uliotengenezwa na Wajerumani, lakini wa sasa umetengenezwa hapahapa nchini. Kwa mujibu wa Abdallah, mfumo huo unatumika katika nchi mbalimbali za Afrika kuendesha mashirika ya treni, lakini mifumo yao ikitengenezwa nje ya nchi.
Tofauti na mifumo hiyo, Tazara imeweka rekodi ya kuwa na mfumo ambao kwa asilimia 70 umeratibiwa na kutengenezwa na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa shirika hilo, wakati asilimia 30 imechangiwa na vijana wengine wa Tanzania. “Hakuna mgeni hata mmoja aliyehusika katika kutengeneza mfumo huu, wote waliohusika ni Watanzania na kwa sehemu kubwa ni vijana wetu hapahapa Tazara,” alisema Abdallah katika mahojiano. Hii inaonesha kuwa, mfumo huo umetengenezwa na Watanzania kwa asilimia 100.
Abdallah alisema tofauti nyingine inayojitokeza kati ya mfumo wa Tazara na mifumo ya nchi zingine ni kuwa wa Tazara umekuwa wa kisasa zaidi kwa kutumia chati inayoonesha mahali halisi na eneo ambako treni ipo. Kutokana na hali hiyo, alisema Tazara ni Shirika la kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kuwa na mfumo unaotumia chati ya kunasa mwenendo wa treni. Teknolojia hiyo inaifanya Tazara kuwa shirika linaloendeshwa kisasa zaidi. Meneja huyo aliyataja manufaa yatakayotokana na matumizi ya mfumo huu kuwa ni usimamizi mzuri wa uendeshaji wa treni. Alisema mfumo huo, una uwezo mkubwa wa kusimamia mwenendo mzima wa treni zinazotembea za abiria na mizigo.
Mfumo huo pia ni msimamizi mzuri wa matumizi ya mafuta ya treni zote za abiria na ya mizigo. Kutokana na uwezo huo, Tazara itaweza kutumia mfumo kudhibiti matumizi ya mafuta kwa treni zake zote. Pia mfumo huo una uwezo wa kusimamia mapato na matumizi ya kampuni. Hii inaweza kuwa faida kwa kampuni katika kudhibiti mapato yake, ikiwa ni pamoja na matumizi. “Kwa kutumia mfumo huu, Tazara inaweza kupunguza gharama kwa kuzuia ubadhirifu kama wa wizi wa mafuta na vinginevyo ambavyo vinaweza kudakwa na kuwekwa wazi,” alisema Abdallah.
Mfumo huu pia unasaidia katika masuala ya ufundi kutokana na uwezo wa kufuatilia utendaji kazi wa injini na mabehewa. Kitendo hicho kinaonesha kuwa mfumo unaweza kubainisha tatizo au hitilafu ya kiufundi inayoweza kujitokeza. Aidha, meneja huyo alisema mfumo huo una uwezo wa kuonesha mahali mabehewa yalipo, ikiwa yanahitajika kuchukua mzigo mahali. Alisema mfumo una uwezo wa kuonesha kuwa ni mabehewa mangapi, hayana mzigo na yatafika muda gani mahali yanapohitajika kuchukua mzigo.
Kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu hao wa Tazara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza menejimenti ya Tazara kubakiza viongozi wenye uwezo wa kuzalisha, kwa lengo la kuongeza ufanisi. Profesa Mbarawa alisema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakati akizindua mfumo huo katika ofisi za Tazara. Aliitaka Tazara itumie mfumo huo kuondoa matumizi yasiyokuwa na msingi, kwani nia ya serikali ni kutaka mashirika yanayojiweza kujiendesha, kujipanga vizuri ili kujitegemea kuliko kutegemea serikali pekee.