Wanawake nchini Rwanda na Kenya ndio wanaotarajiwa kuishi muda mrefu zaidi miongoni mwa wanawake na wanaume katika nchi za Afrika Mashariki, kwa mujibu wa takwimu.

Umri wa wanawake kuishi Rwanda kwa sasa ni miaka 69.3 na nchini Kenya ni miaka 69.0.
Hata hivyo, umri wa kuishi wa wanaume Uganda ndio ulioongezeka zaidi katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, ambapo umepanda kwa miaka 13.5.
Nchini Tanzania, umri wa kawaida wa kuishi kwa wanawake kufikia mwaka 2016 ulikuwa miaka 66, ongezeko la miaka 10 ukilinganisha na mwaka 1990 kwa mujibu wa Utafiti wa Mzigo wa Maradhi Duniani mwaka 2016, ulioratibiwa na Taasisi ya Takwimu za Afya na Utathmini.
Kwa wanaume, umri wa kuishi ulikuwa miaka 62.6 kufikia mwaka 2016 ukilinganisha na miaka 53.7 mwaka 1990. Kwa kiwango cha kadiri, umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kwa miaka kumi kufikia sasa tangu mwaka 1990.
Umri wa kuishi
Nchini Kenya, umri wa kuishi kwa wanawake umeongezeka kutoka miaka 62.6 mwaka 1990 hadi miaka 69 mwaka 2016, ongezeko la takriban miaka sita, lakini kwa wanaume ongezeko limekuwa ni kutoka miaka 60.2 hadi miaka 64.7, miaka 4.5.
Nchini Uganda, umri wa kuishi kwa wanawake sasa ni miaka 64.7 (sawa na umri wa wanaume kuishi Kenya) na kwa wanaume ni miaka 59.8.
Kiwango hicho hata hivyo kimeimarika kwa zaidi ya miaka 10 kwa kila jinsia kwani mwaka 1990 umri wa wanawake kuishi Uganda ulikuwa miaka 52.1 na kwa wanaume 46.3.
Kwa sasa, kwa kawaida, kila mwanamke aliyefikisha umri wa kujaliwa mtoto nchini humo huwapata watoto 4.7 ukilinganisha na watoto 3.7 kwa kila mwanamke Mkenya.
Pato la jumla kwa kila raia Tanzania kufikia mwaka jana lilikuwa $2,516 lakini Kenya lilikuwa $2,925, tofauti ikiwa $409.
Uganda, ambapo pato kwa kila raia kila mwaka ni $1,838, kila mwanamke hujifungua watoto 5.6.

Kinachowaua Watanzania zaidi

Chanzo kikuu cha vifo Tanzania kimesalia kuwa Ukimwi/VVU sawa na ilivyokuwa mwaka 2005, ambapo ugonjwa huo unafuatwa na maambukizi kwenye mfumo wa kupumua mwilini.
Ugonjwa wa Malaria ulikuwa wa tatu kwa kusababisha vifo mwaka 2005 Tanzania lakini sasa nafasi hiyo imechukuliwa na magonjwa ya kuharisha na nafasi ya nne maradhi ya moyo, vyanzo ambavyo mwaka 2005 vilikuwa vinashikilia nafasi ya nne ya tano mtawalia. Ugonjwa wa Malaria unashikilia nafasi ya tano kwa kusababisha vifo nchini humo kufikia mwaka 2016.
Mafuriko Dar es Salaam Novemba 2017Haki miliki ya pichaAFP/GETTY
Ugonjwa wa Kifua kikuu ulikuwa kufikia mwaka 2016 ulikuwa wa sita kwa kusababisha vifo Tanzania, ambapo umepanda kutoka nafasi ya saba mwaka 2017.
Maradhi ya ubongo pia yameongezeka kwa kusababisha vifo katika nafasi ya saba kutoka nafasi ya tisa mwaka 2005, lakini maradhi kichwa baada ya kuzaliwa kwa mtoto yamesalia nafasi ya nane.

Umri wa kuishi kwa wanawake na wanaume baadhi ya mataifa Afrika

TaifaWanawakeWanaume
Afrika Kusini65.559.2
Burundi61.559.2
DR Congo62.760.4
Kenya6964.7
Malawi62.657.9
Misri7569.4
Nigeria66.463.7
Rwanda69.366
Somalia57.756.6
Tanzania6662.6
Uganda64.759.8
Utapia mlo kutokana na ukosefu wa protini na nguvu mwilini ulikuwa nafasi ya sita kwa kuchangia vifo Tanzania mwaka 2005 lakini sasa umo nafasi ya tisa, huku nafasi ya 10, sawa na ilivyokuwa mwaka 2005, ikishikiliwa na visa vya kuzaliwa kwa watoto njiti (watoto ambao hawajafikisha muda ufaao wa kuzaliwa).

Ulemavu

Kwa kusababisha ulemavu, maradhi ya ngozi yanaongoza yakifuatwa na anemia inayosababishwa na ukosefu wa madini ya chuma kwenye damu.
Kisha, yanafuata maumivu ya mgongo na shingo, maradhi ya macho na masikio na matatizo yanayoambatana na mfadhaiko.
Katika nafasi ya sita kuna maumivu ya kichwa, saba kuna ugonjwa wa pumu na nafasi ya nane kuna Ukimwi/VVU. Tisa, ni matatizo yanayohusiana na kuwa na wasiwasi usio wa kawaida na nafasi ya kumi ni ugonjwa wa kifafa.

Kinachowaua Wakenya zaidi

Nchini Kenya, chanzo kikuu cha vifo kimebadilika kutoka Ukimwi/VVU hadi magonjwa ya kuharisha kufikia mwaka 2016, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005 ambapo Ukimwi ulikuwa juu ya magonjwa ya kuharisha.
Magonjwa ya mfumo wa kupumua yamesalia chanzo cha tatu cha vifo Kenya.
Ugonjwa wa Malaria umeshuka sana, miongoni mwa vinavyosababisha vifo Tanzania kutoka nafasi ya 4 mwaka 2005 hadi nafasi ya 11 kufikia mwaka 2016.
Lakini maradhi ya moyo nayo yamepanda kutoka nafasi ya saba kipindi hicho hadi kushikilia nafasi ya nne, ambapo yanafuatwa na magonjwa ya ubongo ambayo yanashikilia nafasi ya tano sawa na ilivyokuwa mwaka 2005. Ugonjwa wa kifua kikuu pia haujabadilika kutoka nafasi ya sita.
Ugonjwa wa matatizo ya kichwa kwa watoto wanaozaliwa, umo nafasi ya saba ukifuatwa na tatizo la kuzaliwa kwa watoto njiti.
Ugonjwa wa meningitis umepanda kutoka nafasi 12 hadi nafasi ya tisa huku nafasi ya 10 ikishikiliwa na utapiamlo wa kukosa protini na nguvu mwilini.

Ulemavu Kenya

Kwa kusababisha ulemavu, maradhi ya ngozi yanaongoza Kenya sawa na ilivyo kwa Tanzania. Hata hivyo, Kenya katika nafasi ya pili yanafuatwa na maumivu ya mgongo na shingo kisha maradhi ya macho na masikio na matatizo yanayoambatana na mfadhaiko nafasi ya nne.
Anemia inayosababishwa na ukosefu wa madini ya chuma kwenye damu inashikilia nafasi ya tano.
Katika nafasi ya sita kuna maumivu ya kichwa, kabla ya Ukimwi/VVU ambao umeshuka kutoka kuwa nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vingi Kenya mwaka 2005.
Mwanamume na rukwamaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Nafasi ya nane ni matatizo yanayohusiana na kuwa na wasiwasi usio wa kawaida, tisa magonjwa ya kuharisha na kumi ugonjwa wa pumu.

Kinachowaua Waganda zaidi

Uganda, chanzo kikubwa cha vifo ni Ukimwi/VVU sawa na ilivyokuwa mwaka 2005, lakini ugonjwa wa kifua kikuu umepanda kutoka nafasi ya nne hadi nafasi ya pili. Ugonjwa wa Malaria ni wan ne, maradhi ya mfumo wa kupumua ya nne na magonjwa ya kuharisha ya tano.
Kenya, ambayo ilikuwa na idadi ya watu 46.6m kufikia mwaka 2016 ilitumia pesa nyingi kidogo kuliko Tanzania iliyokuwa na watu 54.5m kufikia wakati huo kwenye sekta ya afya ambapo ilitumia $8.8B mwaka 2015 ikilinganishwa na Tanzania iliyotumia $8.6B.
Kwa kufuata mfano wa nchi zilizowekeza zaidi katika afya, Tanzania inatakiwa kuwa ikitumia $51.3B nayo Kenya ikitumia $36.6B kufikia mwaka 2040, lakini kwa mujibu wa makadirio ya sasa Tanzania itakuwa ikitumia $31.2B nayo Kenya $21.4B kufikia wakati huo.
Uganda imewekeza sana katika afya na mwaka 2015 ilitumia $13.2B katika sekta ya afya. Kufikia mwaka 2040, taifa hilo likiendeleza mkondo wa sasa, litakuwa linatumia $29.71B ukilinganisha na kiwango kilichopendekezwa cha $29.7B.