Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuwasili nchini Kenya siku ya Jumapili katika ziara ya kibinafsi.
Obama na wageni wake watahudhuria uzinduzi wa Sauti Kuu ,Shirika lisilokuwa la kiserikali la kuwawezesha vijana lililoanzishwa na dadake wa kambo Auma Obama katika eneo la Kogelo kaunti ya Siaya siku ya Jumatatu.
Kabla ya kuelekea Kogelo , Obama na familia yake itamtembelea rais Uhuru Kenyatta na kuonana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Rais Uhuru Kenyatta atamkaribisha Obama katika ikulu punde atakapowasili KenyaHaki miliki ya pichaREUTERS
Maelezo kuhusu kuwasili kwa Obama yamefanywa siri kwa sababu ya maswala ya kiusalama licha ya kwamba kiongozi huyo anatarajiwa kuwasili nchini Kenya siku ya Jumapili jioni.
Hii itakuwa ziara ya nne ya Obama nchini Kenya.

Babake alizaliwa katika eneo la Kogelo mjini Siaya.
Waandalizi wa hafla hiyo wamedai ukosefu wa eneo kubwa la kufanyia sherehe hiyo kuwa sababu kuu ya raia wengi kutoruhusiwa kuhudhuria uzinduzi huo.
''Kutokana na udogo wa eneo, hafla hiyo itahudhuriwa na watu wachache huku vyombo vichache vya habari pia vikiruhusiwa'', ilisema taarifa ya waandalizi,
Mjini Kisumu skrini kubwa zitawekwa katika uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta ili umma kufuatilia ziara hiyo ya Obama.
Siku ya Jumatatu Obama anatarajiwa kuelekea Kisumu ambapo atapokewa na Gavana wa mji huo Anyang' Nyong'o kabla ya kuelekea Siaya.
Atakapowasili mjini Siaya rais huyo wa zamani wa Marekani atapokewa na Gavana wa Siaya Cornel Rasanga kabla ya kusafirishwa hadi katika kijiji cha Kogelo ambako familia yake ya kenya inatoka ili kuzindua wakfu huo wa Sauti Kuu.
Dadake Obama Auma
Image captionObama na wageni wake watahudhuria uzinduzi wa Sauti Kuu ,Shirika lisilokuwa la kiserikali la kuwawezesha vijana la dadake wa kambo Auma Obama
Wawakilishi , wasomi, viongozi wa dini na viongozi wa kijiji walikutana mjini Kogelo siku ya Ijumaa katika kile kiongozi wao alisema kwamba wanajadiliana jinsi ya kumkaribisha bwana Obama.
"Tulikuwa tukijadiliana kuhusu tutakavyomkaribisha. Pia tumejadiliana kuhusu mahitaji ya jamii ambayo tutataka kuwasilisha kwa Obama siku ya Jumatatu, Nicholas Rajula aliambia gazei la Daily Nation nchini Kenya.
''Tunataka kumkaribisha katika kijiji kwa njia ya Kiafrika. Hii itafanyika iwapo kutakuwa na raia wengi. Kwa sababu hiyo tunataka kutoa ombi kwa waandalizi kumruhusu mwana wetu kuhutubia umma kwa ufupi, sio lazima katika eneo la hafla hiyo kwa kuwa ni dogo mno kuruhusu kila mtu kuingia.
Baada ya ziara yake nchini Kenya Obama ataelekea Afrika Kusini.
Hii itakuwa ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu kuondoka madarakani mnamo mwezi Januari 20 mwaka 2017.
Amezuri nchini Kenya mara tatu 1987, 1992 na 2015 wakati alipokuwa akihudumu kwa awamu ya pili ya urais.