Bunge la Sudan Kusini limepiga kura ya kuongeza muhula wa Rais Salva Kiir hadi mwaka 2021 licha ya kushindwa kuandaa uchaguzi wa mwaka huu.
Bwana Kiir amekuwa madarakani tangu Sudan Kusini ipate uhuru wake mwaka 2011 na uchaguzi wa mwaka 2015 nao ulihairishwa.

Hatua hii inahujumu jitihada zinazoendelea za amani zenye lengo la kumaliza karibu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano nchini humo.
Mwezi uliopita Bw Kiir alisaini mkataba na hasimu wake Riek Machar ambapo wote walikubaliana kusitisha kabisa mapigano.
"Msemaji wa serikali awali alisema kuwa wao kama serikali watafanya kila wawezalo kuona kuwa wameongeza muhula wa rais na pengine walikuwa wanaona kuwa ikifika terehe 30 kungekuwa na hali ya kutoelewa kikatiba na kisheria. Kwa hivyo ndipo wakasema kuwa wataongeza muhula huo labda hadi mwaka 2021, lakini watazingatia kuwa wako ndani ya mazungumzo. Lakini hiyo haionyeshi kwamba wao wana picha nzuri kwa upizani na waasi." hii ni kulingana Mohammed Jaffer, mwandishi wa BBC Monitoring aliye na upeo mkubwa kuhusu maswala ya Sudan Kusini.
Makubaliano hayo yalitakiwa kufuatiwa na mazungumzo zaidi na kubuniwa kwa serikali yenye kugawana madaraka, ambapo Machar atateuliwa tena kuwa makamu wa rais huku wanasiasa wengine wakichukua nafasi kwenye baraza la mawaziri.
Wakosoaji wa Bw Kiir wanamlaumu kuwa mtawala wa kiimla anayebakia madarakani kwa nguvu. Anakana madai hayo.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka mwaka 2013 kutokana na uhasama kati ya Bw Kiir na aliyekuwa makamu wake Bw Machar ambaye alikuwa na npango wa kumrithi.
Kwenye taarifa upande wa Riek Machar umetoa malalamiko yake ukisema kuwa utawala wa Sudan hauna haja ya kuwepo kwa suluhu ya amani na pia suluhu kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
Ulisema kuwa makubaliano ambayo yalijadiliwa chini ya usimamizi wa IGAD yangeongeza muhula wa serikali iliyopo na kuashiria mwanzo mpya wa nchi.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa kungeza muhula wa rais sio tu ni siasa mbaya lakini ni pigo kwa imani kati ya pande mbili hasimu na washika dau wengine.