Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage wakijadili jambo wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Jana 10 Julai 2018, Jana 11 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK) 
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akikagua uzalishaji wa sukari wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Jana 10 Julai 2018, Jana 11 Julai 2018. 


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage wakikagua eneo linalo wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Jana 10 Julai 2018, Jana 11 Julai 2018. 

Na Mathias Canal-WK, Misenyi-Kagera



Uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera umeagizwa kuacha urasimu
katika mfumo wa uuzaji wa Sukari wanayozalisha badala yake kuingiza mtaani kwa
wingi Sukari kwa wananchi ili kuepuka kadhia ya upungufu wa huduma hiyo muhimu
katika jamii.

Agizo hilo limetolewa na Mawaziri wa sekta ya Kilimo Mhe Dkt
Charles Tizeba na waziri wa sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles
Mwijage wakati wakizungumza na uongozi wa kiwanda hicho Jana 11 Julai 2018
walipotembela kiwanda cha Sukari wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi
Mkoani humo iliyoanza Juzi 10 Julai 2018.

Mawaziri hao kwa kauli moja wametoa siku 14 kwa kiwanda hicho
kuongeza kasi ya uzalishaji kutoka uzalishaji wa Sukari kwa Tani 350-360 kwa
siku ili kufikia walau Tani 450 mpaka 500 kwa siku kwani kufanya hivyo
wataimalisha uwezo wa Sukari kupatikana kwa wingi kwa wananchi hivyo kuondoa
usumbufu wa gharama katika ununuzi wa bidhaa hiyo.

Aidha, Mawaziri hao wametoa kalipio Kali kwa uongozi wa kiwanda
hicho kwa kuwa na mawakala wachache wa usambazaji wa sukari jambo ambalo
linapelekea ushindani wa kibiashara kuwa mchache mbinu inayopelekea Sukari
kuuzwa kwa gharama isiyokuwa rafiki kwa watumiaji.

Walisema kuwa ndani ya muda mfupi uongozi wa kiwanda hicho
unapaswa kutathmini upya namna ya kuongeza Uwekezaji ili kurahisisha huduma za
wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 hatimaye kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo ifikapo mwaka 2025.

Dkt Tizeba alisema kuwa kumekuwa na uingizaji wa Sukari kwa
magendo kutoka nje ya nchi kwa sababu Viwanda vya Sukari ndani ya nchi
vimefungia sukari kwenye magodaoni bila kuingiza sokoni kwa wingi kuwafikia
watumiaji.

Pia, alisema kuwa wataalamu wa kiwanda cha Sukari wanapaswa kutoa
elimu ya muwa kwa umma ili kuona umuhimu wa uzalishaji wa zao hilo sambamba na
kushirikiana na wakulima wadogo zaidi ya 490 katika vijiji vya jirani na
kiwanda hicho.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage
alisema kuwa serikali inatazama namna bora zaidi ya kukuza takwimu za
uzalishaji wa Sukari nchini hivyo Viwanda vya Sukari vinapaswa kuunga mkono
juhudi hizo kwa kuchochea Uwekezaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Pia alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli haitasita
kuvifungia Viwanda vyote vitakavyobainika kukiuka taratibu, sheria na kanuni za
nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.

MWISHO.