Dkt Charles Tizeba, Waziri wa Kilimo

Na Mathias Canal-WK, Mwanza

"Mhe Waziri Mkuu Jana
tulikuwa na kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania ambalo liliambatana
na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama vya ushirika
kote nchini sambamba na hilo wanachama wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu,


na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa
sekta ya ushirika nchini, nimejiridhisha kwamba kuna umuhimu wa kuwa na somo la
ushirika kwenye mitaala yetu mashuleni" 

Kauli hiyo ilitolewa juzi tarehe
7 Julai 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba wakati akitoa salamu
za Wizara ya Kilimo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa kwenye sherehe za kilele cha siku ya ushirika
Duniani.

Katika sherehe hizo
zilizofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza, Waziri Tizeba alieleza
kuwa changamoto kubwa inayopelekea wananchi wengi kutotambua umuhimu wa
ushirika nchini inasababishwa na kutofahamu tija ya ushirika tangu wakiwa
wadogo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya ushirika chombo ambacho ni
dira na taswita ya mafanikio kwa wakulima.

Aliongeza kuwa miongoni kwa ajenda
muhimu kwake kwa sasa itakuwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Wizara ya
elimu ili kuona namna bora ya kuingiza kwenye mtaala somo litakalohusu ushirika
kwani kufanya hivyo wakulima watapata utambuzi juu ya umuhimu wa ushirika
nchini na hatimaye kuwawezesha kiuchumi.

Alisema kuwa kumekuwa na tatizo
kubwa kwa wakulima, baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika  la kukosa
uzalendo na utambuzi kuhusu ushirika hivyo kudumbukia kwenye wimbi la
ubadhilifu wa Mali za ushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha
wanachama wote.

"Kuingiza ushirika kwenye
mitaala yetu mashuleni kutaibua ufahamu kwa wakulima na kuwaongezea ujuzi kama
ambavyo tumekuwa na somo la stadi za kazi lililowasaidia wananchi kuwa na ujuzi
wa mambo mbalimbali" Alikaririwa Dkt Tizeba

Siku ya ushirika Duniani mwaka
2018 ilipambwa na kauli mbiu isemayo "Ushirika kwa ulaji na uzalishaji
endelevu wa bidhaa na huduma" ikiwa imelenga kukumbusha kwamba vyama vya
ushirika sharti vihakikishe vinajitangaza na kutafuta Masoko ya bidhaa na
huduma zake kwa jamii nzima.

Alisema kuwa pamoja na kwamba
serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika
upatikanaji wa mtaji na kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za kiuchumi katika
kujiendeleza kiuchumi lakini kuongezwa somo la ushirika kwenye mtaala wa elimu
italeta mageuzi makubwa kwa wakulima.

Alisema kuwa pamoja na juhudi
kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili
kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye
vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa
dhana  ya kudhani kwamba vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha
Mazao ya biashara ya nchi za nje lakini juhudi hizo zitakuwa na mabadiliko
chanya zaidi kama ushirika utafundishwa mashuleni.

MWISHO.