Mkuu
wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akizindua jiwe la msingi la kiwanda
kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.

NA DANIEL MBEGA, KISARAWE
MKUU wa Wilaya ya
Kisarawe, Jokate Mwegelo, amepongeza jitihada za akinamama katika kubuni miradi


ya maendeleo na kuongeza kuwa Serikali iko tayari kuunga mkono jitihada zao, na
hasa katika miradi ya kilimo ambayo inaleta uhakika wa chakula.
DC Mwegelo amesema
hayo leo, Jumamosi, Septemba 15, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda
kidogo cha kuchakata muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe,
ambacho kinamilikiwa na akinamama wapatao 30 wanaoongozwa na Ofisa Kilimo
mstaafu, mama Abia Magembe.


Mkuu huyo wa
wilaya aliweka jiwe hilo la msingi kwa niaba ya Waziri wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe.
Alisema anapongeza
jitihada kubwa zilizofanywa na akinamama hao siyo tu katika kubuni miradi ya
maendeleo, bali pamoja na kuwasaidia wengine na kusema kwamba, kiwanda hicho ni
cha mfano ambapo kinakwenda sanjari na kauli mbiu ya Serikali ya kuifanya
Tanzania ya Viwanda.
“Nawapongeza sana
akinamama, pamoja na kiongozi wenu Mama Magembe, hakika hizi ni jitihada
zinazotakiwa kuungwa mkono na serikali yangu itafanya kila njia kuona kwamba
mnasimama,” alisema.
Aliwapongeza pia
wafadhili wa Mradi wa Green Voices waliotoa mafunzo kwa akinamama 15 huko
Hispania, ambapo akinamama 10 kati yao, akiwemo Mama Magembe, walianzisha
miradi ya aina hiyo baada ya kurejea nchini huku wakiwafundisha akinamama
wengine.
Mradi wa Green
Voices, ambao unalenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa
mazingira pamoja na kujikita katika uhakika wa chakula unafadhiliwa na taasisi
ya Women for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania, Maria Thereza de la Vega, ambapo kwa Tanzania akinamama 10
wanaendesha miradi mbalimbali katika mikoa sita.
Miradi mingine ni
utengenezaji wa majiko banifu, ufugaji wa nyuki, kilimo cha uyoga, kilimo
nyumba (green house) cha mboga mboga, ukaushaji wa matunda na mbogamboga kwa
kutumia umeme-jua, kilimo cha matunda, kilimo cha viazi lishe pamoja na
utengenezaji wa majiko ya umeme-jua.
Miradi hiyo iko
katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma na Mwanza.
DC Mwegelo
aliahidi kuwaunganisha akinamama wa kikundi hicho cha Kitanga Green Voices na
taasisi mbalimbali za fedha ili kupatiwa mikopo isiyo na riba au yenye masharti
nafuu, ambapo alisema tayari kikundi kimojawapo kilichopatiwa mafunzo na Mama
Magembe tayari kilikwishapokea kiasi cha shilingi milioni moja kutoka Halmashauri
ya Wilaya.
Alisema, wilaya
yake ina mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata muhogo ili kutengeneza wanga
(starch), lakini kwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha akinamama, anaamini
kinaweza kuwa cha mfano katika kutekeleza maazimio hayo ya serikali.
“Tumepanga
kuanzisha kiwanda cha kuchakata muhogo ili kutengeneza wanga, lakini kwa kuwa
kiwanda hiki kipo, nadhani ni mwanzo mzuri wa kuona kwamba tunaweza kuongeza
nguvu ili azma yetu itimie maana wilaya hii inaongoza kwa kuwa na mihogo
mingi,” alisema.
Akizungumza kabla
ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Mtera Mwampamba,
alisema kwamba muhogo na korosho ni mazao ya kipaumbele katika wilaya hiyo na
kwamba ujio wa kiwanda hicho unaakisi malengo yao.
Awali, Mratibu wa
Kikundi hicho, Mama Magembe, alisema kwamba, fedha walizopewa na wafadhili
zilikuwa takriban shilingi milioni 12 ambazo walizitumia kununulia mashine na
kujenga jengo moja, na familia yake binafsi iliamua kuchangia shilingi milioni
nane ambazo zimejenga jengo la pili pamoja na kununulia matanki mawili ya
kuvuna maji ya mvua.
Hata hivyo, jengo
hilo la pili bado halijakamilika ambapo aliomba serikali iangalie uwezekano wa
kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kusaidia kupatiwa mashine kubwa za kisasa pamoja
na umeme.
“Mbali ya
changamoto ya vitendea kazi na majengo, lakini pia kuna changamoto ya umeme
ambapo tunatumia mashine zinazotumia nguvu kazi za watu, jambo linalokwamisha
uzalishaji wake. Tungekuwa na umeme tunaamini kwamba tungeweza kuzalisha tani
nyingi za unga wa muhogo, lakini pia tukipata mashine kubwa tunaweza kuchakata
muhogo na kuusaga na shughuli nyingine zote zikaishia hapa hapa kuliko ilivyo
sasa ambapo tunalazimika kubeba chenga na kwenda kusaga mjini,” alisema.
Aliitaja
changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa maji safi na salama, hali inayokwamisha
shughuli nyingi.
Hata hivyo, DC
Mwegelo alisema kwamba, mpango wa kupeleka umeme kwenye kijiji hicho upo katika
awamu ya tatu ya Umeme wa REA, lakini akaahidi kufuatilia ili kuona uwezekano
wa awamu hiyo kuanzia kijijini hapo ili kusukuma mbele maendeleo.
Kuhusu suala la
maji, alisema, hivi sasa kuna mpango wa kuleta maji wilayani Kisarawe kutoka
Ruvu, lakini akasema, kwa kuwa maji yatakayozalishwa kila siku kutakuwa na
ziada za lita takriban 2000, wataangalia uwezekano wa kusambaza majji hayo
katika vijiji vingine kikiwemo Kijiji cha Kitanga.
Kuhusu changamoto
ya masoko, DC Mwegelo aliahidi kushirikiana na akinamama hao na wadau wengine
na kuhimiza kwamba, uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na muhogo ndio utakaotoa
fursa ya kupatikana kwa masoko mengi.
DC Mwegelo
alishuhudia bidhaa mbalimbali kama keki, maandazi, tambi, vitumbua, biskuti na
chapatti ambazo zimetengenezwa kwa kutumia unga wa muhogo huku akisema kwamba,
kilimo hicho kikiendelezwa siyo kitakuwa na tija kibiashara tu, bali kitakuwa
na uhakika wa chakula.
Mratibu wa Mradi
wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, aliwashukuru wafadhili wa
mradi huo na kuwapongeza akinamama wote ambao walipata mafunzo na kuja
kuanzisha miradi.
Alisema kwamba,
akinamama hao wameweza kuwapatia mafunzo wanawake wenzao zaidi ya 600 ambao
wako katika vikundi mbalimbali na kwamba miradi mingi imeonyesha mafanikio
makubwa.
Naye Balozi
Getrude Mongella, ambaye ni Mjumbe wa Bosi ya taasisi ya Women
of Africa Foundation,
aliwataka wanawake kote nchini kubuni miradi endelevu na kuwahimiza wanaume
kuwaunga mkono akinamama ili miradi hiyo iweze kufanikiwa.
Kwa upande wake,
mwakilishi wa taasisi ya Women for Africa Foundation, Alicia Cedaba, alisema
kwamba wamefurahishwa na mafanikio katika miradi mingi iliyoanzishwa na
akinamama chini ya ufadhili wao na kwamba wataangalia uwezekano wa kuendelea
kufadhili.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, mara baada ya kuzindua jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe kwa niaba ya Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe. Kushoto ni Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe na kulia ni Balozi Getrude Mongella.
Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe, akimwelekeza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella mara baada ya mkuu huyo wa wilaya kuweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella, wakisikiliza maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe, kuhusu namna muhogo unavyochakatwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia unga wa muhogo uliofungashwa huku akipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia baadhi ya wanakikundi cha Kitanga Green Voices wakiweka mihogo kwenye mashine tayari kwa kuichakata ili kupata chenga pamoja na wanga.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kutokana na unga wa muhogo huku akipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, pia alipanda mti wa matunda katika eneo la kiwanda hicho kidogo kwenye Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation, Alicia Cedaba, akiwa na Mama Abia Magembe, Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices.