MTANGAZAJI wa Clouds,  Soudy Peter  Kadio 'Brown' amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali.

Akisomewa mashtaka na Wakili wa serikali Mkuu Faraja Nguka kwa kusaidiana na wakili Estazia Wilson amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwizile, kuwa kati ya June 11 na September, 2018 ndani ya Dar es Salaam kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Shilawadu Tv mshtakiwa, alitoa maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka (TCRA).

Hata hivyo, mshtakiwa Soudy Brown baada ya kusomewa shtaka hilo amekana na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Wakili Peter Kibatala anayemtetea mshtakiwa huyo aliomba mteja wake apewe dhamana kwa sababu shtaka linalomkabili linadhaminika.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Rwizile amemtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh.Milioni 2, pia mshtakiwa mwenyewe naye asaini bondi ya Sh.Milioni 2.

Mshtakiwa huyo alifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa. Kwa mujibu wa upande wa mashtka, wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi October 18, 2018.

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.