Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba (Mb) akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Leo tarehe 16 Octoba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal,WK)

Kikundi cha ngoma ya asili cha Mkoani Songwe kikitumbuiza mara baada ya waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba (Mb) kuwasili kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Leo tarehe 16 Octoba 2018.
Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba (Mb) akitoa salamu za Rais John Pombe Magufulu wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Leo tarehe 16 Octoba 2018.
Sehemu ya wananchi wakifatilia hotuba ya waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba (Mb) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Leo tarehe 16 Octoba 2018.

Na Mathias Canal-WK,
Tunduma-Songwe

Tanzania imeendelea kuwa ghala
la chakula kwa nchi za jirani kwa kipindi kirefu baada ya kujitosheleza kwa
chakula takribani kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo. 

Tanzania imeweza kuuza ziada ya
mazao mbalimbali ya chakula katika nchi za nje. Kulingana na takwimu
zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kipindi cha mwezi Juni
2017 hadi Juni 2018 yameuzwa mahindi kiasi cha Tani 64,477.95  zenye
thamani ya Shillingi Billioni 90.6  za kitanzania na maharage  Tani
99,434.45 zenye thamani ya shillingi Bilioni 222.0 za Kitanzania. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Kilimo Dkt Charles Tizeba (Mb), Leo tarehe 16 Octoba 2018 wakati akihutubia
mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya
Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika
Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Dkt Tizeba alisema kuwa mazao
hayo yamekuwa yakiuzwa zaidi katika nchi za Kenya, Uganda, DRC, Rwanda,
Burundi, Sudani Kusini na Uarabuni. 

"Pamoja na kuuza mazao nje
ya nchi, nchi yetu imekuwa ikitegemea kuagiza zao la ngano kutoka nje ya nchi
kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo hapa nchini. Serikali inatoa wito kwa
wakulima hususani wa maeneo ambayo zao hili linalimwa na kukua vizuri waweze
kuongeza maeneo ya uzalishaji na tija ili nchi iweze kupunguza utegemezi wa zao
hili kutoka nchi za nje" Alikaririwa akisema

Alisema, Pamoja na uzalishaji
mzuri wa chakula nchini, Lishe duni (utapiamlo) kwa jamii na kwa baadhi ya
maeneo inaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuathiri maendeleo ya
wananchi kiafya, kielimu na kiuchumi.

Aidha, ili kuyafikia malengo
endelevu ya maendeleo (Sustainable Development Goals), alisema , Lishe ni moja
ya muhimili muhimu wa kuwezesha kufikiwa kwa malengo yote 17 hivyo Serikali kwa
kulitambua hilo, imeamua kujumuisha masuala ya lishe kuwa mojawapo ya maeneo ya
kimkakati katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 –
2020/21. 

Kadhalila, aliwataka wadau wote
wa lishe nchini kushiriki na kuonyesha bayana mchango wao katika kukabiliana na
utapiamlo. 

Tarehe 16 ya mwezi Oktoba kila
mwaka, Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, huadhimisha Siku ya
Chakula Duniani ambapo lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kukumbushana wajibu
wa kila mmoja katika kupambana na njaa, kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa. 

Maadhimisho ya mwaka huu
yamebeba kaulimbiu inayosema “ Matendo yetu ni hatima yetu. Dunia bila njaa
ifikapo 2030 inawezekana”. "Kaulimbiu hii inatutaka kufanya kazi
kwa umahiri mkubwa ili tujitosheleze kwa chakula na kuwa na akiba ya kutosha
kuendesha maisha yetu ya kila siku." Alisisitiza Dkt Tizeba na kuongeza
kuwa

"Pia kaulimbiu hii
inatukumbusha kuacha kufanya mambo kwa mazoea na badala yake tutumie utalaamu
katika kuongeza kuzalisha mazao  ya kilimo, mifugo na uvuvi."

MWISHO.