Ni mkutano ambao unafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ukishirikisha vijana viongozi ambao ni wanachama wa vilabu vya Umoja wa Afrika mashariki (EAC) kutoka mikoa 10 ya nchini Tanzania na Zanzibar huku wengine wakiwa wametokea Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Sudani kusini.

Mwandishi wa BBC, Regina Mziwanda aliudhuria mkutano huo ambao umelenga kuwaleta pamoja viongozi vijana kujadili na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na mtengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Na kikubwa zaidi ni jinsi gani vijana wanaweza kushirikishwa na kutoa mchango wao katika kuelemisha wana Afrika Mashariki kuijua Jumuiya yao vizuri.
Licha ya kuwa miunganiko hii ya kikanda imekuwa kwa njia moja au nyingine inashindwa kufikia malengo yake kwa sababu ya ushiriki hafifu wa wananchi na hakuna juhudi za ziada zilizowekwa kuelemisha wananchi.Mkutano huu umelenga pia kuamsha juhudi za kuwapa wananchi uelewa wa kutosha juu ya jumuiya yao.
mkutano
Naibu Waziri wa Vijana nchini Tanzania Antony Peter Mavunde alibainisha mpango wa Tanzania ulioanzishwa kwa ajili ya kuwawekea uwezo kwa sababu kwa mujibu wa utafiti wa 'Inter University council for EA', unasema kwamba asilimia 60 ya vijana wanaomaliza chuo bila ya kuwa na sifa ya kujiajiri au kuajirika.
"Sisi tumelenga kuwafikia vijana zaidi ya milioni 4.4 ifikapo mwaka 2021 ili kuwawekea uwezo vijana wa Tanzania waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine," Mavunde alisisitiza.
Huku kwa upande wao vijana wanaona mikutano kama hii itawawezesha vijana kusaidiana na kushirikiana kwa ukaribu kwa lengo la kukuza jumuiya iwe na umoja.
"Hii ni fursa ya vijana kuweza kuhamasishana kuweza kutembea katika nchi mpaka nyingine," Mwenyekiti wa vijana Afrika Mashariki Gwakisa George Makaranga akizungumza na vijana wa Afrika Mashariki aliieleza BBC.
Sulemani Badru ni kijana kutoka Zanzibar ameeleza namna kiswahili na ufundishwaji wa kiswahili unavyoweza kuwanufaisha vijana wa Zanzibar na Afrika mashariki.
Kwa muujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 inakadiriwa kuwa ni milioni 16.1 ambao ni sawa na asilimia 35.5 ya watanzania wote milioni arobaini na tano.