Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa kuhusu ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia, iliyotokea tarehe 10 Machi 2019 nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

Ndege hiyo ya abiria, aina ya  Boeing 737 yenye namba za usajili ET 302 iliyokuwa inafanya safari zake za kawaida kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea mjini Nairobi, Kenya, ilikuwa imebeba abiria 149 kutoka mataifa mbalimbali na wafanyakazi wa kwenye ndege wapatao 8.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu ajali hiyo, iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia, ikiwemo orodha ya abiria na mataifa wanayotoka, hakuna Mtanzania aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.

Orodha ya nchi na idadi ya raia (kwenye mabano) waliokuwa kwenye ndege hiyo  ni kama ifuatavyo: Kenya (32), Canada (18), Ethiopia (9), China (8), Italia (8), Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7), Misri (6), Ujerumani (5), India (4), Slovakia (4), Austria (3), Urusi (3), Sweden (3), Hispania (2), Israel (2), Morocco (2) na Poland (2).

Nchi zingine ni Ubelgiji (1), Djibouti (1), Indonesia (1), Ireland (1), Msumbiji (1), Norway (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan (1), Somalia (1), Serbia (1), Togo (1), Uganda (1), Yemen (1), Nepal (1), Nigeria (1) na raia aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Umoja wa Mataifa (1).

Mamlaka husika zimeanza uchunguzi ili kujua  chanzo cha ajali hiyo.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na wote walioguswa na msiba huu mzito kutoa pole kwa mataifa yote yaliyopoteza raia wake kwenye ajali hiyo.



Imetolewa na: 
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.

10 Machi 2019