ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,  leo Jumatatu Machi 18, 2019, ametangaza yeye, viongozi na wafuasi wanaomuunga mkono kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.


Maalim Seif ametangaza uamuzi huo ikiwa ni saa chache tangu Mahakama Kuu kumhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa ni Mwenyekiti halali wa CUF,  jambo ambalo Maalim Seif hajaliafiki kutokana na mgogoro uliokuwepo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Machi 18, 2019 mchana katika ofisi za wabunge wa CUF Magomeni jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesema mapambano ya kisiasa lazima yaendelee.

“Mimi na wenzangu, tumetafakari kwa kina juu ya uamuzi wa kesi ulivyokwenda, tumeona kutafuta jukwaa jingine la kulitumia kuwa ni ACT- Wazalendo, nawatangazia Watanzania wote na wanachama wote waliokuwa wanatuunga mkono mimi na wenzangu, tunajiunga na ACT- Wazalendo, tunawaomba wote wajiunge ili kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tumeianza,” amesema Maalim Seif.

Aidha, Maalim amewashukuru wote waliojitolea nyumba zao kwa ajili ya ofisi za CUF na kuomba waendelee kufanya hivyo wakiwa ACT- Wazalendo.
“Mapambano ya kujenga demokrasia sio kazi ya nyepesi, tumefanya kazi kubwa hadi hapa tulipofikia,” amesema.

Maalim amedai tukio hilo ni historia mpya kwa Zanzibar na Bara na kwamba “umma haujawahi kushindwa kokote duniani, ndiyo historia inaonyesha, hatuna wasiwasi kuwa umma wa Watanzania nao utashinda.”

Kuhusu kuhama na nyadhifa zake, Maalim Seif amesema wanahamia huko pasina masharti wala vyeo na wanakwenda kama wanachama wa kawaida na ikiwa watapewa vyeo watavichukua au la.
Akizungumzia nafasi ya wabunge wa chama hicho amesema ni wana CUF, wengi wanawaunga mkono wao lakini wamewaachia wenyewe, kama watahama sasa au baadaye.

BREAKING : MAALIM SEIF Ahamia ACT Wazalendo kuungana na Zitto