Yametimia hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya msanii maarufu wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ’Harmonize’ kumvalisha pete ya uchumba msanii wa Bongo Movie, Kajala Masanja.

Tukio hilo limefanyika leo Jumamosi Juni 25,2022 hoteli ya Serena na kulipa jina la ‘Late Lunch’ huku likihudhuriwa na watu wa karibu wa wasanii hao ukiwemo uongozi wa lebo ya Konde Gang, Mkurugenzi wa TVE, Francis Ciza ’Majizo’, Aunty Ezekiel, Martin Kadinda na wengineo.

Wawili hao wamechumbiana ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu walipotengana baada ya mwanamuziki huyo kumfungulia mashtaka Kajala na binti yake Paula akiwatuhumu kuvujisha picha zake za utupu.

Kwa upade wake Kajala amesema: “Hakuna asiyejua tuliyoyapitia, pia mimi si mkamilifu so nikaona kwa nini nisimsamehe, So Harmonize naahidi  nitakupenda leo, kesho hadi milele,”.

Mahusiano ya wawili hayo yalijulikana rasmi Februari mwaka jana, lakini ilipofika Aprili lilisambaratika baada ya kuvuja kwa picha za utupu ambazo Harmonize ilielezwa alimtumia mtoto wa mpenzi wake huyo.

Akizungumza kabla ya kumvalisha pete, Harmonize amesema wamepitia mengi na msanii huyo na anashukuru hatua hiyo waliyofikia.Aidha amesema kwa wasiojua yeye na Kajala wamejuana zaidi ya miaka saba iliyopita tangu akiwa hana pa kulala mpaka kupata mafanikio aliyonayo leo.

“Mimi na Kajala tuna historia ndefu ,tulijuana miaka saba iliyopita, nililala kwake nkiwa sina pa kulala mpaka leo mnaponiona hapa,”amesema.