Chini ya jua kali la Tanzania, Lossim Lazzaro anatazama shamba lake kwa hofu.

Anamwaga samadi ya mifugo polepole kwenye mazao yake, katika jaribio la mwisho la kuyasaidia kukua.

Bw Lazzaro anamiliki ekari tano za ardhi na aliwahi kuwa mkulima wa nyanya aliyefanikiwa katika mkoa wa kaskazini wa Arusha. Lakini sasa, kama wengine wengi, anapambana kuweka biashara na mimea yake hai, huku kukiwa na uhaba wa mbolea duniani.

"Imekuwa vigumu kwangu kupata mbolea sokoni," Bw Lazzaro anasema.

Mbolea - kiungo muhimu kinachohitajika kusaidia mazao kukua - haipatikani kote ulimwenguni.  Bei za kimataifa pia zimepanda kwa kiasi fulani kutokana na mzozo wa Urusi na Ukraine.

"Nilikuwa nikinunua mbolea kwa takriban dola 25 kwa kila mfuko wa kilo 50 mwaka  2019," Bw Lazzaro anakumbuka.

"Lakini mfuko huo sasa unauzwa  karibu mara mbili ya bei hiyo, ni ghali sana kwangu."

Kiasi cha mbolea kinachopatikana duniani kimekaribia kupungua kwa nusu, wakati gharama ya baadhi ya aina ya mbolea imeongezeka karibu mara tatu katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Hilo linaleta athari kubwa katika nchi kama Tanzania, ambako wakulima wanategemea mbolea kutoka nje.

"Niliishia kununua mbolea kutoka kwa mtengenezaji wa ndani lakini bado nililazimika kuagiza miezi mapema kutokana na uhaba," Bw Lazzaro anaongeza.

Mkulima wa tomato Tanzania
Maelezo ya picha,

Mkulima wa tomato Tanzania Lossim Lazaro

Mahitaji ya mbolea inazozalishwa ndani ya nchi yanaongezeka. Wakulima wadogo kaskazini mwa Tanzania sasa wanageukia maeneo kama vile Minjingu Mines and Fertilizer Ltd, mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mbolea nchini.

Kampuni hiyo inasema inakabiliwa na ongezeko la ghafla la mahitaji na inajitahidi kutimiza maagizo. Lakini wakuu wanasema hawawezi kuongeza uwezo wao kutokana na ushuru mkubwa.

“Hatuna usawa ukilinganisha na waagizaji,” alisema Tosky Hans, Mkurugenzi wa Minjingu Mines and Fertilizer.

"Wazalishaji wa ndani wanapaswa kulipa kodi nyingi, ambayo waagizaji hawalipi," aliongeza.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi, wawekezaji wa kigeni wanapewa ruzuku nchini Tanzania ili kuvutia uwekezaji huku wazalishaji wa ndani wakilipa kodi iliyowekwa.

Muungano wa (Agra), shiŕika lisilokuwa la kiseŕikali ambalo linakuza suluhu za kijani kibichi katika bara zima, linasema hii ni fuŕsa kwa wakulima kuweza kujitegemea zaidi.

Vianey Rweyendela, meneja wa Agra Tanzania, anahimiza wakulima kuungana na kuunda vyama vya ushirika, hatua ambayo anasema inaweza kuwapa sauti kuhusu bei ya soko.

"Hilo litawasaidia kuwa na uwezo wa kujadiliana na mbolea itakayouzwa kwao itakuwa nafuu," anasema Bw Rweyendela.

Bei ya ngano imesababisha kila kupanda bei nchini humo

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Bei ya ngano imesababisha kila kupanda bei nchini humo kutoka mkate hadi noddles

Mtu tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, hivi majuzi alizindua kiwanda cha mbolea nchini Nigeria, ambacho kinatarajiwa kuzalisha tani milioni tatu za mbolea ya urea kila mwaka.

Anaamini, uzalishaji wa hakika utaleta mabadiliko.

“Kuagiza mbolea na kuifikisha imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima barani Afrika na hatimaye kukosa msimu wao wa upanzi,” anasema Bw Dangote.

"Kwa kuzinduliwa kiwanda hiki, tutahakikisha wakulima wanapata virutubisho mapema."