Msemaji wa Yanga, Haji Manara ameripotiwa kufunguliwa shauri mbele ya kamati ya maadili iliyochini ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF)  kutokana na kile ambacho kilitokea jana, Jumamosi kwenye mchezo wa fainali ya ASFC.

Awali ilionekana jana kwenye video fupi iliyosombaa kwenye mitandao ya kijamii kutokea uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Ofisa huyo wa Yanga akitupiana maneno na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia.

Lakini mara baada ya mchezo wa fainali ambayo Yanga ilitwaa taji lao la tatu msimu huu, Manara alitumia ukurasa wake wa Instagram kueleza juu ya kile ambacho kilitokea huku akikanusha madai ya kumtukana rais huyo kama ilivyokuwa ikilezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Leo, Jumapili TFF imetoa taarifa ya kwamba Sekretarieti yake imefungua shauri mbele ya Kamati ya maadili dhidi ya Ofisa huyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kwenye klabu ya Simba.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba, "Kamati ya maadili kupitia kwa Mwenyekiti wake, tayari imepewa taarifa kuhusu malalamiko dhidi ya Manara, hivyo itapanga siku ya kusikiliza shauri hilo na malalamikiwa atapewa taarifa."

"TFF inawakumbusha wanafamilia ya mpira wa miguu kuwa wanabanwa na katiba na kanuni mbalimbali za mchezo huo, hivyo wanatakiwa kuwa makini kwa vitendo na kauli zao kuhusu mpira wa miguu."