Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia alikuwa Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, amevuliwa wadhifa huo na wabunge wenzake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Chama hicho ambacho kimeunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, zilithibitisha jana kuwa wabunge hao waliokuwa wamekutana Bagamoyo kwa siku tatu, walimvua Zitto wadhifa huo wa Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kuwa alikiuka makubaliano ya pamoja ya wabunge hao.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi na wabunge hao walipokutana kwa ajili ya kujengewa uwezo wa namna ya kuuliza maswali bungeni, kujenga hoja na kuzijua kanuni za Bunge.
Taarifa hizo zilieleza kuwa sababu kubwa iliyofanya Zitto aenguliwe kwenye nafasi hiyo ni uamuzi wake wa kupingana na wabunge wenzake nje ya kikao kilichoamua kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, alipokuwa akilizindua Bunge la 10, Novemba 18, mwaka huu. Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, wakati akivuliwa nafasi hiyo alikuwa nje ya kikao hicho baada ya kutoa udhuru wa kutohudhuria kwa maelezo kwamba alikuwa anaenda hospitalini kwa matibabu.
Akizungumza jana, Zitto ambaye amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, alisema hakuwa amepewa taarifa rasmi kutoka kwenye chama juu ya kuvuliwa nafasi hiyo. Zitto ambaye amelazwa chuma namba 57 ghorofa ya tatu hospitalini hapo, alisema:
“Nafasi hii sikugombea kwa hiyo kama chama kinaihitaji ni suala tu la kuniambia kwamba wanayahitaji hayo madaraka sio kukaa na kupigakura.” NIPASHE ambayo ilifika hospitalini hapo kumjulia hali, alisema anasumbuliwa na maumivu ya tumbo na homa ambayo ilimuanza juzi usiku alipokuwa Bagamoyo kwenye kikao cha wabunge wote wa chama. Alisema kwa sasa ana nafuu, lakini anasubiri majibu ya vipimo zaidi. Mbunge mwingine wa Chadema ambaye naye anasumbuliwa na tumbo ni Said Arf wa Mpanda Mjini ambaye naye amelazwa hospitalini hapo.
Arf pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara. Akizungumza hospitalini hapo jana, Arfi alisema anasumbuliwa na tumbo na tayari amefanyiwa vipimo ambapo madaktari wamemshauri aende nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
“Nimeshauriwa niende nje kwa hiyo kesho (leo), nitaenda India kwa matitabu,” alisema Arf.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo, hakukanusha wala kuthibitisha na kuahidi kuzungumza baadaye, lakini alipotafutwa simu yake ya mkononi haikupatikana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alipoulizwa alisema “Sijapokea taarifa hizo kiofisi lakini hayo yanawahusu wabunge itapendeza sana kama wao watakujibu,” alisema. Uamuzi huo umefikiwa wiki kadhaa baada ya Zitto na wenzake tisa kutoingia bungeni Novemba 18, mwaka huu wakati wabunge wa Chadema walikuwa wameafikiana kwa kura, kuwa watoke nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Kikwete akizindua Bunge. Pamoja na makubaliano hayo, Zitto na wabunge hao hawakuingia bungeni.
Wengine ambao hawakuonekana siku hiyo ni Arfi, Mhonga Luhwanya (Viti Maalum), John Shibuda (Maswa Magharibi), Maulida Komu (Viti Maalum), Profesa Kulikoyele Kahingi, (Bukombe), Rachel Mashishanga (Viti Maalum), Raya Ibrahimu (Viti Maalum), Lucy Owenya (Viti Maalum) na Suzan Lyimo (Viti Maalum).
0 Comments