Mawaziri, Manaibu, wanajeshi na maelfu ya wananchi wameuaga mwili wa Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), William Kotta katika ibada iliyofanyika kwenye kanisa la Anglikana la Mtakatifu Alban lililopo jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa washiriki hao ni Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Regnald Mengi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernald Membe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka na Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Lazaro Nyalandu.habari zaidi..
Kotta alifariki ghafla nyumbani kwake eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam, Desemba 6 mwaka huu, baada ya kupata mshituko wa moyo.
Ibada hiyo iliongozwa na Padri Joseph Soseleje, aliyesema kifo cha Kotta ni pigo kubwa kwa jumuiya ya kanisa hilo, kwa vile alikuwa mshauri wao na kwamba alichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao.
"Kwa kweli tumepata majozi makubwa kutokana na kwamba alikuwa ni mtu mwema ambaye anajitolea kwa watu wote bila kuchagua, alikuwa mshauri wetu hivyo ana ushuhuda mkubwa ambao unatakiwa kuigwa," alisema Padri Soseleje
Padre Soseleje alisema kifo cha Kotta kimetoa fundisho kwa watu, kwamba wanatakiwa kuwa na ushuhuda ulio na matendo bora, ili uweze kuigwa katika jamii na taifa.
Alifafanua kuwa pamoja na kwamba marehemu huyo alihama eneo lake la kuishi kutoka Oysterbay kwenda Mbezi, waliendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kimaendeo ikiwemo kushauriana katika masuala ya kanisa.
Alisema kutokana na kwamba alionyesha uaminifu mkubwa na ndipo walipomfuata na kumuomba awe mshauri wa kanisa la Anglikana la Kawe.
Naye mtoto wa marehemu Kotta, Steve Kotta alisema kuwa baba yake alifariki ghafla baada ya kupata mshutuko wa moyo.
Alisema baba yake ameacha watoto sita na wajukuu 10, na kwamba mama yao alishafariki miaka miwili iliyopita.
Alisema baba yao watamkumbuka kwa mambo mengi ambayo amewatendea pamoja na wananchi wengine ambao alikuwa akiwasaidia katika misaada tofauti.
Kwa mujibu wa Steve, Kotta alijiunga JWTZ mwaka 1966 ambapo alikuwa katika kikosi cha kupiga mizinga na kwamba alistaafu mwaka 1997.
Alisema baada ya hapo marehemu alijishughulisha na biashara mbalimbali kama vile kuanzisha benki ya Azania, kampuni na kuwa mshauri wa kanisa.
Baada ya kuagwa mwili wa marehemu katika kanisa hilo, ulichukuliwa na kupelekwa Lugalo kwa ajili ya wanajeshi kutoa heshima zao za mwisho na hatimaye kwenda kuzikiwa katika kiwanja chake huko Goba jijini hapa.