Rais Jakaya Kikwete amekutana rasmi kwa mara ya kwanza na Baraza la Mawaziri jipya pamoja na Naibu Mawaziri na kuwapa maelekezo ya awali ya nini anakitarajia kutoka kwao.
Mawaziri wote 29 na Naibu Mawaziri wote 21 ambao Rais Kikwete aliwaapisha rasmi kushika nyadhifa zao katika sherehe iliyofanyika Jumamosi iliyopita, walihudhuria mkutano huo kwenye Chumba cha Baraza la Mawaziri, Ikulu, Dar es Salaam.
Rais aliwaeleza mawaziri kuwa katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wake hakutakuwepo na muda wa kupoteza, na wala hatakuwa tayari kukubali maelezo ya kwa nini utekelezaji wa majukumu ya msingi umeshindikana.
Aliwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri hao akisisitiza: Nimewateua kwa imani kuwa pamoja nanyi, tutatimiza matumaini ya wananchi wa Tanzania waliokichagua Chama Cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi yetu.”
Rais Kikwete aliwaelezea majukumu yao na kutaka kila Waziri ahakikishe anatayarisha kalenda yake ya masuala muhimu ambayo anataka yajadiliwe na Baraza la Mawaziri kwa mwaka.