Mwanasheria mkongwe Zanzibar, Awadhi Ali Said amesema sheria namba 11 ya mwaka 1985 ya karafuu inayowalazimisha wakulima kuuza zao hilo serikalini, inakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu. Aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akitoa mada juu ya haki za binadamu katika.habari zaidi soma....
Mwanasheria mkongwe Zanzibar, Awadhi Ali Said amesema sheria namba 11 ya mwaka 1985 ya karafuu inayowalazimisha wakulima kuuza zao hilo serikalini, inakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.Aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akitoa mada juu ya haki za binadamu katika kongamano la kuadhimisha Siku ya haki za binadamu duniani lililooandaliwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar.
Kongamano hilo lilifanyika chini ya uenyekiti wa Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina Peter, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ZLSC, ujumbe wa mwaka huu ‘Kemea-Komesha aina zote za uzalilishaji’
Alisema kwamba sheria hiyo inawanyima haki wakulima wa zao la karufuu kuuza zao lao wanapotaka, wakati wakulima wa mazao mengine Zanzibar wanaruhusiwa kuuza mazao yao nje ya soko la serikali.
Awadhi alisema sheria hiyo inastahili kuangaliwa upya kwa vile kitendo cha kuwalazimisha wakulima kutumia soko moja kimesababisha kudorora kwa uzalishaji wa zao hilo, ambalo siku za nyuma lilikuwa linaoongoza kwa kulipatia fedha za kigeni taifa la Zanzibar.
Alisema ni jambo la kushangaza wakullima wa mazao ya aina mbali mbali Zanzibar, likiwemo la viungo wanaruhusiwa kutumia masoko wanayotaka na ambayo yana bei nzuri kuliko soko la serikali.
Akifafanua, Awadhi alisema kuwanyima wakulima wa karafuu kuuza mazao yao kwa njia ya soko huria na kuwaruhusu wakulima wa mazao mengine kufanya hivyo, ni ubaguzi wa hali ya juu.
Alisema wakati umefika sheria hiyo kufutwa ikiwa ni hatua ya kuondoa ukiritimba wa shirika la biashara la taifa ZSTC kumiliki soko la zao hilo na pia ni njia ya kulinda haki za binadamu.
Alisema inashangaza wakulima wa karafuu wanapotafuta soko linalotoa bei nzuri kwa zao hilo, wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kufanya biashara ya magendo.
Alisema kutokana na hali hiyo uzalishaji wa zao hilo umeshuka kutoka tani 14,000 hadi tani 3,000 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 1970 na 1980.
Hata hivyo alisema suala la ukiukaji wa haki za binadamu linaweza kudhibitiwa Zanzibar iwapo kila mwananchi kwa nafasi yake atashiriki katika kupiga vita vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kwa jumla.
Akichangia mada hiyo, Mwanadiplomasia mstaafu, Mohamed Yusuf alisema Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la umaskini kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ufisadi na rushwa kuchukua nafasi kubwa miongoni mwa baadhi ya watendaji na viongozi.
Alisema baadhi yao wanamiliki mali za kutisha, zikiwemo nyumba za kifahari na shule, huku mitaji yao ikiwa haijulikani ilivyopatikana na hakuna mtu anayethubutu kuhoji suala hilo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali Uki alisema Zanzibar inakabiliwa na tatizo la kutoa ajira kwa misingi ya ubaguzi na kwamba tatizo hilo linasumbua wananchi katika nchi nyingi barani afrika.
0 Comments