Pambano hilo ni maalum kwa ajili ya kutangaza aina hiyo mpya ya mchezo wa ngumi ambao unajumuisha aina tofauti za mapigano kuanzia ngumi, mateke, karate, kukabana, mieleka na kadhalika.
Akizungumza jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Katibu wa Chama cha Ngumi Mseto nchini (TMFA), Shomari Kimbau alisema pambano hilo litakuwa ni la kwanza kufanyika nchini na tayari sheria zake zimeshatambulishwa rasmi katika mazoezi yaliyohusisha mabondia mbalimbali.
Shomari alisema kuwa anaamini aina hiyo mpya ya ngumi itaibua vipaji zaidi kwa sababu vijana wengi wamekuwa wakipigana mitaani na sasa wamepata mchezo unaotambulika kisheria na TMFA imeuanzisha ili kuvutia mabondia wengi kuucheza.
"Lengo letu la kuanzisha mchezo huu ni kutaka watu wengi wajifunze mchezo ambao mara nyingi umekuwa ukichezwa mitaani bila ya wachezaji kupata faida na baadhi yao kufikishwa katika vyombo vya sheria," aliongeza.
Alisema kutokana na hali hiyo, aliona ni vyema akaandaa pambano hilo ili kuwatambulisha wachezaji wa mitaani kuwa aina hiyo ya mchezo ni ajira hivyo ni bora wachezaji wake wakapata mazoezi na kupigana katika ulingo ili kujipatia fedha.
Alisema pambano hilo litakuwa na raundi tano na limeandaliwa chini ya Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini (TPBO).
Alisema mbali ya pambano hilo, kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi ya ndondi za kawaida likiwemo la kuwania ubingwa wa taifa wa uzito wa kati litakalowahusisha mabondia, Thomas Mashali dhidi ya Said Mbelwa.
Mapambano mengine yatakuwa ni kati ya Francis Miyeyusho dhidi ya Fabian Lampard wakati Yohana Robert atapigana na Kalaghe Suba huku Tanganyika Tyson atapanda ulingoni kumvaa Matiku Magesa.
Bondia chipukizi Paulo David naye atavaana na Ramadhani Kido katika pambano jingine la uzito wa kilo 80.
0 Comments