Wanafunzi 37,947 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu mkoani Dar es Salaam, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, huku wengi wao wakiwa wanatoka katika shule za Wilaya ya Kinondoni.
Kati ya idadi ya waliofaulu, wavulana ni 19,833 na wasichana ni 18,114, ambao ni sawa na asilimia 65 ya watahiniwa wote 58,219 waliofanya mtihani mkoani humo.habari zaidi.....
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Elia Ntandu, alisema jana kuwa katika idadi hiyo, Kinondoni imeongoza kwa kuwa na watahiniwa 15,523 ikifuatiwa na Temeke yenye watahiniwa 12,453 na Ilala 9,971 waliofaulu mtihani huo.
“Kutokana na hali hiyo Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam zitakuwa zimewapatia nafasi ya kidato cha kwanza wanafunzi wote waliofaulu,” alisema Ntandu. Alisema wanafunzi waliofanya mtihani huo, ni 58,219 na kwamba idadi hiyo inahusisha pia wanafunzi wa shule zisizo za serikali.
Ntandu alisema kati ya wanafunzi waliotahiniwa, wavulana ni 28,322 na wasichana 29,897 sawa na asilimia 97 ya wanafunzi wote waliosajiliwa kufanya mtihani huo, ambao walikuwa 59,820.
Kaimu Katibu Tawala huyo alisema wanafunzi 1,601 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali, zikiwamo utoro, ugonjwa, vifo, mimba na wengine kuhamia mikoa mingine.
Alisema kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, 46 wamechaguliwa kujiunga na shule zinazochukua watoto wenye ufaulu mzuri, ambao wavulana ni 31 na wasichana 15.
Ntandu alisema jumla ya wanafunzi 55, wamechaguliwa kujiunga na shule za ufundi za bweni, kati yao, wavulana wakiwa ni 52 na wasichana ni watatu.
Alisema vile vile wanafunzi 24 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni kawaida, wavulana wakiwa 14 na wasichana 10.
Ntandu alisema wanafunzi 1,960 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kutwa za serikali zilizoko Dar es Salaam, wavulana wakiwa ni 740 na wasichana 1,220.
Alisema wanafunzi 35,834, wakiwamo wavulana 18,984 na wasichana 16,850, wamechaguliwa kujiunga na shule 123 za sekondari zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.
Ntandu alisema wanafunzi 28 wenye mahitaji maalum, wamepangwa shule za bweni za serikali kuu zinazochukua wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Kwa kuwa shule nyingi za wananchi ziko nje ya Jiji, halmashauri za manispaa zote tatu zimeandika barua kuomba wanafunzi watakaokosa nafasi kwenye kata wanazoishi wapangwe kwenye shule zenye nafasi nje ya kata zao,” alisema Ntandu.
Alisema kutokana na maombi hayo, wanafunzi 14,027 wamepangwa nje ya kata zao, kati yao wavulana wakiwa ni 7,751 na wasichana 6,837.
Ntandu alisema katika idadi hiyo, ndani ya halmashauri, Ilala wamepangwa wanafunzi 4,527, wavulana wakiwa ni 2,430, wasichana 2,398; Kinondoni wanafunzi 4,742, wavulana 2,607 na wasichana 2,395; Temeke wanafunzi 4,758, wavulana 2,714 na wasichana 2,044.
Aliwashauri wazazi/walezi kushiriki kuziendeleza shule hizo ili ziweze kutoa elimu bora zaidi na siyo kuwahamisha wanafunzi hao.
Alisema ufanisi uliopatikana, umetokana na jitihada za uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwezesha mkoa kuwa na shule za sekondari 123 zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.