MEDANI ya soka nchini imepata pigo lingine kutokana na kifo cha kiungo mahiri wa zamani wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Nicodemus Bambanga.

Kifo hicho cha Bambaga kimekuja wiki chache baada ya kiungo mahiri wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Juma Mkambi naye kufariki dunia, ambapo kabla ya Mkambi pia aliyepata kuwa kocha mahiri nchini, Syllersaid Mziray naye alifariki dunia.
Kwa mujibu wa mpwa wa marehemu, Marwa Kasuhu, Bambanga alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Lugalo,Dar es Salaam alikokuwa amelazwa tangu Jumamosi iliyopita kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kifua kubana na hali yake ilibadilika juzi saa tano usiku na kuaga dunia.

Bambaga alipata kuchezea Pamba ya Mwanza, Yanga na Simba zote za Dar es Salaam, Malindi na Mlandege za Zanzibar na kung’ara pia na Taifa Stars. kwa habari zaidi....
Kwa mujibu wa mpwa huyo, Bambaga ameacha mjane na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 11 ambaye anasoma shule ya msingi Gilman Rutihinda, Kigogo jijini Dar es Salaam.

Alisema taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu Kigogo na mwili unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda kijijini kwao Mwisenge, Musoma mkoani Mara kwa ajili ya maziko, ambayo yanatarajiwa kufanyika Jumamosi.

“Bambaga kabla ya kufariki, alisema watu wasihangaike kumsafirisha wanaweza kumzika popote, lakini shangazi zake pamoja na mjomba wake wamesisitiza akazikwe nyumbani Mwisenge ambako ndiko asili ya wazazi wake ambao wote wamekwishatangulia mbele za haki,” Kasuhu alisema, Bambanga aliyezaliwa mwaka 1964 Mwisenge, baada ya kustaafu soka Nico alikuwa akijishughulisha na biashara mbalimbali.

Wakimzungumzia Bambanga wachezaji ambao wamewahi kucheza naye katika timu mbalimbali, walibainisha kuwa watamkosa kiungo huyo kwa mambo mengine hasa tabia yake ya uungwana pamoja na uongozi wake katika masuala mbalimbali.

Mshambuliaji Edibily Lunyamila ambaye alicheza na marehemu Yanga na Malindi, alisema licha ya kucheza naye waliishi katika nyumbani moja hapo kabla na kusema kuwa Bambanga alikuwa ni mtu makini na mkimya ambaye ukigombana naye basi lazima chanzo cha ugomvi utakuwa wewe.

Na kwa upande wake Bitta John yeye alimtaja Bambanga kama mtu ambaye alimshawishi ajiunge na timu ya Pamba wakati akiichezea, lakini alikuja kujiunga naye wakati akiwa Simba na Taifa Stars ambako alikuwa kiongozi wake katika mambo mbalimbali .

Baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwanye msiba huo jana ni pamoja na Abdallah Msamba, Abubakari Kombo, Athumani Jumapili Chama, Robert Damian na Dua Said ambaye ni jirani yake marehemu.