Hospital ya Regency kwa kushirikiana na wataalamu wa saratani kutoka India, kesho (Jumatatu) wanaendesha kambi ya bure ya uchunguzi wa maradhi ya saratani.
Kambi hiyo ya siku mbili itaendeshwa katika hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam na bingwa wa maradhi ya saratani kutoka India, Dk Sridhar P S kutoka HCG group mji wa Bangarole India.kwa habari zaidi
Mwenyekiti wa hospitali hiyo, Dk. Rajni Kanabar, alisema jana kuwa uchunguzi huo utafanywa kwa kushirikiana na wataalamu kutoka taasisi ya Health Care Global Group, Bangalore India.
Dk. Kanabar alisema taasisi hiyo ni kubwa katika kutibu maradhi ya saratani kusini na mashariki mwa bara la Asia.
Alisema wagonjwa watakaokutwa na matatizo watapewa ushauri wa kitaalamu kwa saratani za mapafu, mifupa, saratani ya tezi na ile ya damu.
“Watakaokuwa na matatizo makubwa watapelekwa taasisi ya saratani ya Ocean road lakini wenye matatizo madogo madogo watatibiwa hapa hapa Regency, uchunguzi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa wa saratani kwa kupata ushauri wa kitaalamu kwa mtaalamu bingwa kutoka India,” alisema Dk. Kanabar.
“Wale watakaokuwa na matatizo makubwa sana ambao hawataweza kutibiwa hapa Tanzania watapelekwa hospitali ya HCG Group ya mji wa Bangalore kwa gharama ndogo sana kama tulivyokubaliana kati ya Regency na wao,” alisema.
Alisema ushirikiano baina ya hospitali hizo unatarajia kufanikisha kujengwa kwa kituo cha aina yake cha utafiti wa saratani jijini Dar es Salaam.
Alisema chini ya ushirikiano huo, wataalamu wa saratani kutoka Marekani, India na Afrika Kusini watakuwa wakija nchini kwa makubaliano maalum na kutibu wagonjwa hapa nchini kwa gharama nafuu.
Alisema utaratibu huo utaiwezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kutibia wagonjwa wa nchini hapa ambao wana matatizo makubwa ya saratani na kusaidia kuokoa fedha nyingi za kigeni kwenda kutibu wagonjwa nje ya nchi.
0 Comments