NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kabwe Zitto amefunua mdomo wake na kueleza kuwa hana sababu ya kujiuzulu nafasi hiyo, huku akiwataja baadhi ya watu anaohusishwa kuwa na ukaribu nao, kwamba anafanya hivyo kwa sababu ya
maslahi ya Taifa na ya jimbo lake.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, akiwa ni kijana na mahiri wa kujenga hoja, amesema hatajiuzulu kwa sababu Chadema ni chama cha utetezi kwa wananchi wa Mkoa wa
Kigoma.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya CINE ATLAS Ujiji katika Manispaa ya Kigoma juzi, Zitto alisema baadhi ya watu wanaona amefanya kosa kubwa
ambalo kama si kufukuzwa, basi anapaswa kujiuzulu; jambo alilosema kwa upande wake, haoni kosa lolote ambalo amefanya hadi sasa.

Kuhusu tuhuma za kushirikiana na kuzungumza na viongozi mbalimbali akiwamo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Rais Jakaya Kikwete, alisema amekuwa akizungumza na watu hao kwa maslahi ya Taifa na maslahi ya wananchi wa jimbo lake na Mkoa wa Kigoma.

Akibainisha sababu za kuwasiliana na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, alisema alifanya hivyo pale ilipotokea zahama ya kupigwa mabomu akiwamo yeye, kwenye ofisi za
Mkoa za Chadema mjini hapa.

Alisema hakuna kosa kuzungumza na watu hao kama ziko sababu za kuzungumza nao, na kufafanua kuwa tofauti za kiitikadi, siyo uadui na kuwafanya wasiwasiliane hata kwa masuala muhimu ya wananchi.

Akimzungumzia Rais Kikwete, alisema ni kiongozi wa kitaifa na kama ipo fursa ya kukutana na
kuzungumza au kuwasiliana naye, siyo kosa kufanya hivyo na hasa kwa mustakabali wa wananchi wa jimbo lake.