WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema, serikali haina kigugumizi wala ugumu katika mjadala unaoendelea sasa nchini kuhusu Katiba mpya na atamshauri Rais Jakaya Kikwete namna ya kushughulikia madai hayo.
Aidha, amesema mchakato wa kuwapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi, lakini kwa kuzingatia utaratibu utakaofaa bila kuathiri sheria zilizopo, unaendelea na siyo kwamba suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi. Amesema, atamshauri Rais Kikwete kuhusu namna bora ya kushughulikia madai ya Katiba mpya, huku msimamo wake ukiwa ni kuundwa kwa jopo la wataalamu kutoka kada zote za maisha au kuwashirikisha wananchi wenyewe katika kueleza nini kifanyike kuhusu Katiba mpya.
Mbele ya wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake Magogoni, Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu alikiri kuwapo kwa mjadala mkali unaoendelea kuhusu Katiba mpya, lakini akasema si vyema kuona kuwa madai hayo si ya msingi, hivyo ni vyema kuheshimu mawazo ya watu wanayoyatoa.
“Kumekuwapo na mjadala mkali kuhusu Katiba mpya. Moja niseme kwamba tusione kama madai haya si ya msingi, tuheshimu mawazo yanayotolewa, kila mmoja awe huru. Lakini tatizo limekuwa labda katika uwasilishaji wake,” alieleza Waziri Mkuu katika mkutano aliouitisha na wanahabari.
“Serikali haina kigugumizi katika suala hili, wala ugumu. Hapana. Sasa limeiva na mimi nitalichukua na kuona njia bora ya kulifanyia kazi.
Nitamshauri Rais kama kuunda kikundi cha wataalamu kwa ajili ya kukusanya maoni hayo, na kisha kulipeleka katika Bunge kwa sababu ni wawakilishi wa wananchi, au kufanya mjumuiko wa watu wote, huko lijadiliwe kwa uzito wake na jamii. Tutaona litatufikisha wapi.”
Alisema kwake anaamini kuwashirikisha wanazuoni ndio njia safi, huku akisisitiza kuwa maoni yanayotolewa sasa bado yanaweza kuboreshwa kwa sababu baadhi yanatolewa yakionekana kama vile Tanzania haijawahi kuwa na Katiba, au ina Katiba ya hovyo isiyo na mambo mema.
“Ukisikiliza ni kama vile hakuna Katiba kabisa nchini au kuna Katiba ya hovyo…kama vile hakuna mema yaliyotufikisha hapa, yapo mema mengi sana,” alisema Waziri Mkuu, akitolea ufafanuzi wa hoja iliyoibuka mara baada ya uchaguzi mkuu ya kutaka kuwapo kwa Katiba mpya.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kilishindwa katika uchaguzi mkuu kwa nafasi ya urais, kimekuwa kikishinikiza kuwapo kwa Katiba mpya, hoja ambayo imeungwa mkono na vyama vingine vya siasa, wanazuoni, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na baadhi ya wananchi.
Waziri Mkuu alisema Tume mbili, ile ya aliyekuwa Jaji Mkuu Francis Nyalali ya mwaka 1991 na ya mwaka 1996 ya Jaji Mstaafu Robert Kisanga maarufu kama White Paper, vilikuwa na maoni mazuri na viliacha baadhi ya viporo, kwa hiyo, kwa maoni yake, viporo hivyo vinaweza kuwa mwanzo wa kuanzia kuhusu Katiba mpya.
Katiba ya Tanzania iliandikwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977, ingawa ilianza kutumika mwaka 1961 na kuwapo Katiba ya muda mwaka 1965. Tangu mwaka 1977, imekuwa ikifanyiwa marekebisho na hadi sasa ni takribani mara 14 imefanyiwa marekebisho hayo, na siyo kuandikwa upya.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Waziri Mkuu alisema mchakato wa suala hilo unaendelea na ulisimama wakati wa uchaguzi mkuu tangu kuundwa kwa jopo linalowashirikisha wataalamu wa serikali na wanazuoni chini ya mwavuli wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Alisema kimsingi, kazi ya jopo hilo ni kushughulikia jinsi gani Mahakama ya Kadhi itafanya kazi zake nchini bila kuathiri sheria zilizopo nchini, na vikao vitaanza tena muda si mrefu.
“Mtazamo wa serikali haujabadilika…tunachofanya ni wao kuwa na mfumo wao, chombo chao, kwa utaratibu wao. Kazi ya serikali ni kushauri. Kwangu mimi, Waislamu wanastahili kuwa na Mahakama yao ya Kadhi, hamuwezi kuniambia kuwa hawastahili, hapana.
Kazi yetu ni kuhakikisha linafanyika kama yalivyo madhehebu mengine,” alifafanua Waziri Mkuu.
Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu Mahakama ya Kadhi tangu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilipoliweka suala hilo katika Ilani yake ya Uchaguzi ya 2005-2010 ambapo ilieleza kuwa itaweka mazingira mazuri ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, na Waziri Mkuu, alisema ndicho inachokitekeleza sasa.
0 Comments