Serikali ya Sweden kupitia shirika lake la maendeleo na ushirikiano (SDC), imekubali kuipatia asasi ya Foundation for Civil Society Dola za Marekani 3,636,000 (Sh. bilioni 5.16) katika kipindi cha mwaka 2010-2013, kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kuwa na nguvu ya kuleta mabadiliko katika utawala wa kidemokrasia nchini.
Lengo lingine la msaada huo, ambalo ni kati ya malengo yaliyobuniwa na asasi hiyo, ni kuwawezesha Watanzania kupiga vita umaskini na kufikia maisha bora kwa kila Mtanzania.
Mkakati huo unatarajiwa kufikiwa kupitia Asasi za Kiraia (AZAKi) kwa kuzipatia ruzuku na kuzijengea uwezo, hivyo kuzifanya kuwa chachu ya mabadiliko na mchakato wa maendeleo.
Makubaliano ya ufadhili huo, yalitiwa saini Desemba 14, mwaka huu kati ya Mkuu wa Ushirikiano wa SDC, Carin Salerno na Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society, John Ulanga.
Katika makubaliano hayo, SDC itatoa kiasi ilichoahidi kwa awamu katika kipindi hicho, hivyo kuchangia katika kusaidia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Foundation wa miaka mitano kuanzia mwaka 2009.
Serikali ya Uswisi ni miongoni mwa wafadhili wakubwa, ambao wamekuwa wakiisaidia asasi hiyo tangu kuanza shughuli zake nchini mwaka 2003, ambapo hadi mwaka jana ilikuwa imeshaisaidia Dola za Marekani milioni 5.1 (Sh. bilioni 7.23).
Rais wa asasi hiyo, Dk. Stigmata Tenga na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Prudence Kaijage, waliishukuru serikali ya Uswisi kwa kuendelea kuisaidia asasi hiyo na hivyo kuwawezesha Watanzania kushiriki vyema michakato ya sera na utawala inayochangia kuinua hali zao za maisha.
Asasi hiyo ilianzishwa mwaka 2002 kama chombo cha kujengea uwezo asasi za kiraia za Tanzania. Tangu kipindi hicho, imesaidia zaidi ya asasi za kiraia 2000 nchini kote kwa kuzipatia ruzuku na misaada mingine ya kujengea uwezo inayofikia thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 (Sh. bilioni 42.54).
0 Comments