WACHEZAJI wa Yanga jana waligomea mazoezi wakishinikiza uongozi uwalipe fedha zao za usajili wanazoidai klabu hiyo.
Juzi wachezaji hao walizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kusema kwamba wameamua kufikia uamuzi wa kugoma kutokana na ahadi waliyopewa ya kumaliziwa fedha zao zilizobaki kutotekelezwa, huku tayari wakiwa wameshaugawa msimu.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana jioni zilisema kuwa wachezaji hao walifika kama kawaida kwenye Uwanja wa Uhuru ambapo kocha mkuu pia Kostadin Papic alikuwepo lakini badala yake hawakuingia uwanjani kama inavyotakiwa bali walipanda kwenye gari na kuamua
kuondoka.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alikiri kutokea kwa sakata hilo na kuwalaumu wachezaji kuwa kitendo walichokifanya si cha kiungwana.
“Ni kweli wanadai lakini njia waliyoitumia kudai haki yao si ya kiungwana wangetafuta utaratibu mwingine wa kufanya hivyo”.
Habari zaidi zinasema, wachezaji hao wametishia kutocheza hata mechi ya kirafiki ya kesho dhidi ya AFC Leopard ya Kenya.
Inadaiwa kuwa fedha zote za wachezaji wanazoudai uongozi zinafika Sh milioni 70 na kwamba waliahidiwa wangelipwa Novemba 15, lakini imekuwa kimya na wao suala hilo tayari wameshalifikisha kwa kocha.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Afrika Kusini alipo kwa mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Davis Mosha alisema taarifa hizo zinamchanganya na kushusha lawama kwa mfadhili Yusuf Manji.
“Unajua tatizo ni kwamba sisi tulipochaguliwa timu tuliikuta, hivyo kuhusu malipo yao ya usajili walipatana na mfadhili na yeye ndio anatakiwa kuwalipa, sasa hajalitekeleza hilo,” alisema.
“Kwa sasa inakuwa ngumu kufanya uamuzi wowote kwani watu wote hatupo, tupo likizo, mimi nipo huku, Mfadhili nae yuko likizo, Mwenyekiti naye yuko huko, ningewaomba wavute subira ili tukirudi tuangalie namna ya kufanya,” alisema.
Gazeti hili lilifanya jitihada kumtafuta Manji ili kulitolea ufafanuzi suala hilo lakini halikufanikiwa.
0 Comments