Baraza la Taifa la Mitihani (Nacte), limewafutia matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba watahiniwa 88 wa Shule ya Msingi Nyangao iliyopo Jimbo la Mtama mkoani hapa kwa madai ya kuwa matokeo yao yalifanana.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Joseph Mnyikambi wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali mwakani baada ya kufaulu mtihani huo.habari zaidi gonga chini...
Mnyikambi alisema ofisi yake imepokea kutoka baraza hilo ikielezea taarifa zisizoridhisha zinazohusiana na tuhuma za udanganyifu kwa shule mbalimbali za msingi mkoani humo ikiwemo ya Nyangao.
Alisema shule hiyo iliyopewa namba PS 0802105 wakati wa kusahihisha mitihani hiyo iliyofanyika mwaka huu ilibainika watahiniwa wote 88 wakiwemo wawili walemavu wasioona, majibu yao yamefanana.
Alisema walemavu hao walikuwa na alama zinazofanana kwa karibu masomo yao yote.
Mnyikambi alifafanua katika somo la Kiswahili walipata alama 43, Kingereza 40, maarifa ya Jamii 40, Hesabati 38 na Sayansi 39 huku majibu ya kukosa na kupata yakifanana kwa watahiniwa wote.
Ofisa elimu huyo alikiambia kikao hicho kuwa kuna dosari chache zilijitokeza wakati wa kufanya mitihani hiyo kwa shule za msingi za Kilwa, Lindi Vijijini, Nachingwea na katika Manispaa ya Lindi.
Wanafunzi 18,271 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu, 17,938 wakiwemo wavulana 10,201 na wasichana 7,674 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika sekondari za serikali za kutwa mkoani hapa mwakani.
0 Comments