Kiongozi wa upinzani wa siasa za Kiislamui nchini Sudan , Hassan al-Turabi, amekamatwa na vikosi vya usalama nyumbani kwake, kwa mujibu wa chama chake.Katibu wake , Awad Babiker, ameliambia shirika la habari la Reuters, maafisa wa usalama wakiwa na silaha waliwasili nyumbani kwake wakiwa ndani ya magari kadhaa.
Kwa mujibu wa Bwana Babbiker, vikosi vya usalama pia vilimkamata mmoja wa wasaidizi wa Bwana Turabi baada ya kutokea mapambano.
Siku ya Jumaapili, Bwana Turabi alionya kuzuka kwa "mapinduzi ya umma" ikiwa serikali haitaondoa hatua mpya za kubana matumizi.
Bwana Turabi, aliyekua mshirika wa karibu wa Rais Omar al-Bashir, ameshawahi kuwekwa kizuizini mara kadhaa tangu alipounda chama cha Popular Congress Party (PCP).
Aliwahi kuwekwa kizuini kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu mwaka 2010, baada ya kurudia madai kwamba uchaguzi wa mwezi wa Aprili ulifanyika kwa njia ya hadaa.
Siku ya Jumaatatu Bwana Turabi alionya uasi kama uliotokea nchini Tunisia wiki iliyopita "unaweza kutokea Sudan wakati wananchi wana hasira kuhusu kiwango cha umasikini, ukosefu wa marekebisho na hofu kuhusu uwezekano wa kujitenga kwa Sudan Kusini, akiongeza kusema "Sudan sio nchi ndogo kama Tunisia, lakini inakabiliwa na vurugu hata kushinda zile za Somalia"
Siku ya Jumaapili vyama vya upinzani viliitisha mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kuwapongeza wananchi wa Tunisia na kudai "utawala wa mabavu wa Khartoum utokomezwe".
0 Comments