Mshambuliaji wa timu ya soka ya wanawake ya Mburahati Queens FC ya Tanzania, Asha Rashid anayechezea pia timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania- Twiga Stars, amewasili Istanbul, Uturuki, tayari kujiunga na klabu ya soka ya wanawake ya Atasehir Belediyespor, inayocheza ligi kuu ya soka ya wanawake Uturuki.(Pichani Asha rashidi kushoto akiwa na Raisi wa klabu ya Atasehir,Sadiki Kayhan).
Iwapo Asha atafanikiwa katika upimaji wa afya yake na kupatiwa kibali cha kufanya kazi na serikali ya Uturuki, ataingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo.
Klabu hiyo ya Atasehir Beladiyespor wanaongoza ligi ya wanawake ya nchi hiyo na iwapo watamudu kushikilia nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu huu utakaomalizika mwezi wa Mei, watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kutafuta bingwa wa UEFA kwa vilabu vya Ulaya kwa wanawake msimu wa 2011/12.
Wakala wa FIFA, Ahmet Goksel Arici, mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa ya Uturuki, ndiye aliyewaona Asha na mwenzake wanaocheza wote Twiga Stars, kupitia video ya Youtube. Akaituma video hiyo kwa meneja wa timu ya Atasehir, Murat Ulku, ambaye haraka akafanya mipango ya kuwachukua wachezaji hao. Akiwa amevutiwa na usakataji soka wa akina dada hao wa Tanzania, Ulku akawatumia mwaliko Asha na Eto Mlenzi anayechezea timu ya JKT Queens. Chini ya wiki moja, Asha alipata visa ya Uturuki na tayari yupo Istanbul, huku mwenzake Eto akiwa na matumaini ya kujiunga naye, akisubiri ruhusa ya likizo kutoka klabu ya JKT Queens. Asha kwa sasa haruhusiwi kucheza hadi atakaposajiliwa rasmi na Shirikisho la Soka la Uturuki, lakini amefanya mazoezi na timu hiyo na kuwavutia kutokana na uhodari wake wa kupiga mikwaju.
Ingawa hadi sasa Asha hajacheza mechi yoyote na klabu hiyo, amekuwa kivutio kikubwa miongoni mwa mashabiki wa Atasehir, waliokuwa wakimshangilia na kuimba jina lake. Timu hiyo ina matumaini makubwa na mchezaji huyo.Asha mwenyewe amesema anajiamini na matumaini yake ataisaidia timu yake na ameshaangalia soka ya Uturuki na hakuna kitakachombabaisha.
0 Comments