Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLCS), Ishaaq Ismail Sharif, katika mahojiano maalum na NIPASHE kuhusiana na hukumu hiyo, ambapo alisema misingi ya haki za binadamu inakataza matumizi ya nguvu na mateso katika ukusanyaji wa ushahidi.
Alisema tangu kukamatwa kwa Mtanzania huyo mwenye asili ya Zanzibar huko nchini Pakistan mwaka 2004, alishikiliwa kwa muda mrefu na Shirika la Upeleleza la Marekani (FBI) na baadaye kuhamishiwa katika gereza la mateso lililopo Guantanamo, ambako alilalamika kukutana na vitisho na mateso makubwa.
Sharif, alisema kwa msingi huo, adhabu ya kifungo cha maisha gerezani iliyotolewa dhidi ya Ghailan ni batili, kwa vile ushahidi uliotumika kumtia hatiani hauwezi kusimama mbele ya sheria kutokana na kutumika kwa nguvu na mateso wakati wa ukusanyaji wa ushahidi huo.
“Katika misingi ya kisheria, ushahidi unaokusanywa kwa kutumia nguvu au mateso, hauwezekani kumwingiza hatiani mshtakiwa, kwa sababu ushahidi huo hauna nguvu katika kutoa hukumu” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Aidha, alisema kesi hiyo haikupaswa kusikilizwa na mahakama za kiraia za Marekani na badala yake ilipaswa kusikilizwa katika mahakama za kimataifa, ikiwemo ya ‘The Hauge’, kwa vile haiwezekani Marekani ikawa mkamataji na wakati huohuo ikasikiliza kesi na kutoa hukumu.
Naye Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mbwezeleni, alisema ushahidi wowote unaokusanywa kwa kutumia njia za kumfinya mshtakiwa, haukubaliki mbele ya mahakama, lakini alisema jambo la msingi ni kuangaliwa taratibu za kisheria kama zilizingatiwa katika kesi hiyo.
Alisema ushahidi wa kukusanya kwa kutumia nguvu, hauruhusiwi kwa sababu unamuathiri mtuhumiwa kiakili, na unaweza kumtia mtu hatiani bila ya kuwa na kosa, ingawa alisema kwamba nchi nyingi zimekuwa zikitumia ushahidi wa kutumia nguvu hasa katika kesi za uhalifu mkubwa kama vile matumizi ya silaha.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Eric Holder, alikaririwa na vyombo vya habari vya kimataifa, akisema kifungo cha maisha kilichotolewa na Jaji Lewis Kaplan, kimeonyesha uwezo wa mfumo wa sheria wa Marekani katika kuwawajibisha magaidi kwa vitendo vyao.
0 Comments