Awali ilitangazwa mechi hiyo ilitangazwa kwamba ingechezwa kesho kwenye uwanja wa Uhuru kama ambavyo jana mchana Afisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alivyotangaza akisisitiza kwamba hayo ni maamuzi rasmi ya klabu.
Akizungumza jana katika makao makuu ya klabu ya Yanga, Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema kuwa kiingilio cha juu katika eneo la VIP A katika mchezo huo ni Sh. 20,000, VIP B ni Sh. 10,000 na mashabiki watakaotaka kukaa kwenye viti vya rangi ya machungwa watalipa Sh. 5,000.
Sendeu alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri ambapo wamejipanga kuwa makini kutokana na wapinzani wao nao kutokuwa timu ya kuidharau.
"Tumejiandaa vyema na mchezo huu wa kimataifa hasa ukizingatia ushindi wa mechi zetu mbili za Ligi Kuu ya Tanzania Bara tulioupata umesaidia kuimarisha morari ya wachezaji wetu, hatuidharau Dedebit kwa sababu ina nyota wanaochezea timu yao ya taifa na mchezaji mwingine mmoja kutoka Ghana," alisema Sendeu.
Aliongeza kuwa wageni wao wanatarajiwa kuwasili nchini kesho alfajiri huku pia waamuzi na kamisaa wa mchezo huo, Linekela Hafeni Temba kutoka Namibia pia akiwasili kesho hiyo hiyo.
Aliwataja waamuzi watakaochezesha mchezo huo ambao wamepangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa ni mwamuzi wa kati, Abd Elgadir Eldin, atakayesaidiana na Mohammed El Tom Aarif na Saeed Salim Mohammed wote kutoka Sudan.
Hata hivyo, Sendeu alisema kuwa timu yao itahamisha kambi yake leo kutoka klabuni kwao na kwenda 'mafichoni' kwa maandalizi zaidi.
Yanga ambayo ndio kinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara watarudiana na Wahabeshi hao kati ya Februari 11 na 13 mjini Addis Ababa, Ethiopia na mshindi atakutana na Haras El Hadoud ya Alexandria, Misri.
0 Comments