Rais Jakaya Kikwete, amesema msimamo wa Tanzania ni wazi kabisa kwamba haikubali mgombea ambaye kila ushahidi unaonyesha kuwa alishindwa uchaguzi kuendelea kushikilia madaraka.
Rais anayekubaliwa kimataifa kuwa alishindwa uchaguzi mkuu wa Novemba, mwaka jana nchini Ivory Coast, Laurent Gbagbo, amekataa kukabidhi madaraka ya kuongoza nchi hiyo kwa Alassane Quattara, ambaye anakubaliwa kimataifa kuwa alishinda uchaguzi huo kwa asilimia tisa.
Kwa upande wake, Ban Ki Moon alisema vitendo na maamuzi ya Gbagbo tangu ashindwe uchaguzi wa nchi hiyo, vinahujumu mamlaka, madaraka na nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kulinda na kutetea demokrasia na haki duniani.
“Inawezekana vipi, ushindi wa asilimia tisa wa Quattara ukabadilishwa na kuwa ushindi wa asilimia moja wa Gbagbo?” Alihoji Ban Ki Moon katika mazungumzo hayo.
Ban Ki Moon ameutaka Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas), kushirikiana kuhakikisha kuwa demokrasia inadumishwa nchini Ivory Coast.
Aidha, Rais Kikwete, pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Marekani (Usaid), Dk. Rajiv Shah, mjini Geneva, Uswisi.
Rais Kikwete yuko mjini Geneva kuhudhuria na kuendesha mkutano wa kwanza wa Tume ya Kimataifa Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto ambako yeye ni Mwenyekiti Mwenza na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper.
Ban Ki Moon alikuwa mjini Geneva kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano wa Tume hiyo inayoongozwa kwa pamoja na Rais Kikwete na Waziri Mkuu Harper wakati Dk. Shah ni Kamishna katika Tume hiyo yenye makamishna 30.
0 Comments