MAREKANI imetambia mfumo wake wa sheria kuwa unafanya kazi baada ya kumhukumu kifungo cha maisha jela Mtanzania Ahmed Ghailani (36) aliyepatikana na hatia ya kula njama za kufanya uharibifu na kuharibu mali za Marekani kwa milipuko. Hukumu dhidi yake ilisomwa juzi jijini New York, Marekani katika mahakama ya kiraia na Jaji Lewis Kaplan. Ghailani alipatikana na hatia Novemba mwaka jana baada ya kufutiwa mashitaka ya mauaji ambayo awali pia yalikuwa yakimkabili.
Hata hivyo baada ya hatua hiyo, Baraza la Congress lilimzuia Rais Barack Obama kuwahamishia Marekani wafungwa wa gereza la Guatanamo.Kwa mujibu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana, mashitaka yaliyokuwa yakimkabili Ghailani yanahusu milipuko ya mabomu katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998.
Jijini New York juzi, Jaji Lewis Kaplan alikataa ombi la Ghailani la kumsamehe, akisema mateso yoyote ambayo anadai aliyapata akiwa mikononi mwa polisi “hayalingani na mateso na hofu aliyosababisha kwa watu wengine akishirikiana na wenzake.
“Kosa hili lilikuwa kubwa,” alisema. “Yalikuwa ni mauaji makubwa na aliwasababishia ulemavu watu wasio na hatia kwa kiwango kisichomithilika.”
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Eric Holder, alisema kifungo cha maisha kimeonesha uwezo wa mfumo wa sheria wa Marekani katika kuwawajibisha magaidi kwa vitendo vyao.
“Tunatumaini kwamba kifungo hiki cha maisha jela ni kipimo cha haki kwa waathirika wa mashambulizi haya na familia zao na marafiki ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu siku hii,” alisema kwenye taarifa yake.
Ingawa adhabu hiyo haikuwa ikitarajiwa na Wizara ya Sheria nchini Marekani, kifungo cha maisha kwa Ghailani kimechukuliwa na Holder kama kigezo cha kuonesha nguvu za mahakama za Marekani.
Lakini ni vigumu kuona ni lini kesi ya mfungwa mwingine wa Guantanamo itakaposikilizwa, au lini hasa Rais Obama atalifunga gereza la kijeshi la Guantanamo Bay.
Wiki kadhaa baada ya Ghailani kupatikana na hatia mwishoni mwa mwaka jana, Baraza la Congress lilipitisha sheria inayozuia fedha za Jeshi kutumika kuhamisha wafungwa wa Guantanamo kuwapeleka Marekani.
Hiyo inasababisha ugumu kwa utawala wa Obama ‘kulisafisha’ gereza hilo na kuwahamishia wafungwa na kuwashitaki katika mahakama za kiraia.
“Kutokana na hali ilivyo, hatutaacha kuwafikisha magaidi wanaotaka kudhuru watu wa Marekani mbele ya vyombo vya sheria, na tutatumia kila uwezo uliopo serikalini kufanya hivyo,” alisema Holder.
Kabla ya hukumu, Ghailani aliomba asamehewe au apunguziwe adhabu, akisema hakuwahi kudhamiria kuua mtu yeyote na kwamba aliteswa mikononi mwa polisi.
Mwaka 2001 watuhumiwa wanne waliokula njama hizo walihukumiwa kifungo cha maisha jela kutokana na mashambulizi hayo ya Agosti yaliyosababisha vifo vya watu 224.
Waendesha mashitaka walisema Ghailani alikula njama na wafuasi wa kikundi cha al-Qaeda kushambulia balozi hizo kwa mabomu, na alisaidia kununua milipuko hiyo ambayo ilitumika kuharibu ubalozi wa Dar es Salaam, Tanzania.
Wapelelezi wa Marekani walisema Ghailani alikimbilia Pakistani usiku wa mkesha wa mashambulizi hayo yaliyopishana muda mfupi.
Alishitakiwa Marekani Desemba 1998 lakini akajificha Afghanistani na Waziristani nchini Pakistani, Marekani inasema. Alikamatwa Julai 2004 na kuhamishiwa Guantanamo Bay mwaka 2006.
Mwaka jana, Marekani ilisimamisha kesi katika mahakama ya kijeshi ya Guantanamo Bay na kumhamishia New York na kushitakiwa kiraia. Ghailani mwenye umbo fupi, anaelezwa kuwa na majina mengi ya bandia yakiwamo ya ‘Fupi’ na ‘Ahmed Mtanzania’.
Alikuwa mtu wa nane katika orodha ya watu waliokuwa wakisakwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Alituhumiwa kununua lori lililotumika kubebea bomu lililolipua ubalozi wa Dar es Salaam. Yeye na washirika wake pia walikuwa wakituhumiwa kununua matangi ya oksijeni na acetylene yaliyotumika kuchachua mlipuko huo.
Pia anadaiwa kumsindikiza mtengenezaji wa bomu hilo kati ya Dar es Salaam na Mombasa, Kenya, baada ya bomu hilo kutengenezwa na pia kuuchunguza ubalozi wa Marekani akiwa na dereva wa lori hilo.
Mabomu hayo mawili yaliyofuatana kulipuka yaliua watu 213 Nairobi na 11 Dar es Salaam na kujeruhi maelfu.
Kwa mujibu wa nyaraka za Marekani kumhusu Ghailani, anadaiwa kukiri kutembelea kambi ya mafunzo ya al Qaeda iliyoko Afghanistani baada ya milipuko hiyo.
Lakini alikana kuwa mwanachama wa kikundi hicho. Ghailani anaripotiwa kuwahi kuwa Monrovia, Liberia mwaka 2001, akifuatana na mtuhumiwa mwingine wa milipuko hiyo, Mkenya Fazul Abdullah Mohammed.
Gazeti la Observer la Uingereza mwaka 2002 liliripoti kwamba wawili hao walikuwa wakiendesha operesheni hatari za al Qaeda huku wakiuza almasi bandia na kujipatia fedha.
Lilisema operesheni hiyo iliingia matatani Juni 2001 taarifa zilipoifikia al Qaeda, kwamba Ghailani na Mohammed walikuwa wakitapanya fedha kwa wanawake, zawadi na pombe.
Ghailani ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar alikamatwa Julai 25, 2004 nchini Pakistan akiwa na mkewe raia wa Uzbekistani.
0 Comments